Na Mwandishi Wetu
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imetoa msaada wa mashine mbili za kisasa za kutoa joto kwa watoto njiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana.
Msaada huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini, hususan kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa taasisi hiyo kurejesha kwa jamii kupitia michango ya watumishi wake.
Mashine hizo zinatarajiwa kusaidia kuokoa maisha ya watoto njiti kwa kuwapatia joto muhimu katika hatua za awali za uhai wao.
Amesema hadi sasa taasisi hiyo imefikia hospitali 17 kati ya 26 zilizopangwa kunufaika na mpango huo.
“Tunendelea kuhakikisha tunafikia maeneo yenye uhitaji mkubwa zaidi ili kusaidia kuokoa maisha ya watoto,” amesema Chalamila.
Ameongeza kuwa TAKUKURU imeona umuhimu wa kusaidia watoto njiti ambao wanahitaji uangalizi maalum ili kuongeza nafasi yao ya kuishi.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Amana, Jumanne Ihoyelo, amesema mashine hizo zitasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa vifaa tiba.
Amesema pia zitachangia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa watoto njiti hospitalini hapo.
“Vifaa hivi vitaboresha huduma na kusaidia kupunguza vifo vya watoto njiti vinavyoweza kuzuilika,” amesema Ihoyelo.
Naye Muuguzi Mwandamizi wa wodi ya watoto, Mary Machemba, ameishukuru TAKUKURU kwa msaada huo muhimu.
Amesema msaada huo utasaidia kuokoa maisha ya watoto wengi zaidi wanaohitaji huduma za karibu.
Aidha, ametoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia sekta ya afya ili kuboresha huduma kwa watoto na makundi mengine yenye uhitaji mkubwa.






Post a Comment