TCB YAZINDUA KAMPENI YA KUCHOCHEA UCHUMI NA KUWEZESHA NDOTO ZA WATANZANIA


 *******

Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imezindua kampeni maalum yenye lengo la kuimarisha ujumuishwaji wa kifedha na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kuwawezesha Watanzania kupata suluhisho sahihi za kifedha. 

Hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa makundi mbalimbali, hususan wajasiriamali na biashara ndogo na za kati, ili kuchangia ukuaji wa kipato na ustawi wa jamii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo jijini Dar es salaam  Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TCB Bank, Kaimu Mkurugenzi Jema Msuya, amesema benki hiyo imejipanga kuwa mshirika wa kimkakati katika maendeleo ya kiuchumi kwa wateja wake kwa kuwapatia huduma zinazowawezesha kufanikisha malengo yao ya kifedha,amesisitiza kuwa upatikanaji wa huduma bora za kifedha ni nyenzo muhimu katika kukuza uzalishaji, uwekezaji na ajira.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa TCB Bank, Alex Dwashi, amesema kampeni hiyo inalenga kujenga uhusiano wa karibu na wateja kwa kuelewa mahitaji yao na kutoa suluhisho mahususi yatakayosaidia kukuza shughuli za kiuchumi, ameeleza kuwa benki hiyo inaendelea kupanua huduma zake ili kugusa sekta muhimu kama kilimo, biashara ndogo na za kati pamoja na familia, hatua itakayoongeza mzunguko wa fedha katika uchumi.

Naye Meneja Mwandamizi wa TCB Bank, Al-Amin Lwano, amesema utekelezaji wa kampeni hiyo utahusisha kuwafikia wajasiriamali moja kwa moja katika maeneo yao ya biashara ili kuwapatia mikopo na huduma za kifedha zinazolenga kuongeza mtaji na ufanisi wa uzalishaji,ameongeza kuwa uwezeshaji wa wajasiriamali una mchango mkubwa katika kukuza pato la taifa, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi endelevu wa wananchi.









0/Post a Comment/Comments