TOZO MPYA ZA BANDARI ZIFUTWE KABISA-TACAS

.........

Wafanyabiashara na wadau wanaotumia Bandari ya Dar es Salaam wameiomba Serikali kuondoa kabisa tozo mpya za maboresho ya miundombinu ya bandari zilizotangazwa hivi , wakidai kuwa zinaweza kuongeza gharama za biashara na hatimaye kuumiza walaji wa mwisho.

Wadau hao wameeleza kuwa licha ya uamuzi wa mamlaka ya Bandari kusitisha kwa muda tozo hizo hadi Julai 1 mwaka huu, bado kuna haja ya kuzifuta kabisa na kuweka utaratibu mpya utakaokuwa rafiki kwa pande zote zinazohusika katika shughuli za bandari.

Maoni hayo yametolewa na wanachama wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TACAS) wakati wa Mkutano Mkuu Maalum uliofanyika Februari 13 jijini Dar es Salaam kujadili masuala mbalimbali yanayogusa sekta ya forodha na biashara kupitia bandari.

Wakizungumza katika mkutano huo, wadau hao wamesema tozo hizo zinaweza kuwa mzigo mkubwa kwa mawakala wa forodha, wafanyabiashara pamoja na walaji wa mwisho kwa kuwa gharama zake zitaongezwa kwenye bei ya bidhaa ili wafanyabiashara wasipate hasara.

Aidha wameeleza kuwa endapo tozo hizo zitaendelea kutozwa bila marekebisho, kuna hatari ya baadhi ya wafanyabiashara kuhamishia mizigo yao katika bandari za nchi jirani ili kupata unafuu wa gharama, hali ambayo inaweza kuathiri ushindani wa bandari za Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Wadau hao wamependekeza kuwepo kwa mfumo mpya wa utozaji unaozingatia ushirikishwaji wa pande zote muhimu ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mamlaka ya Bandari Tanzania, mawakala wa forodha pamoja na wafanyabiashara, ili kuhakikisha tozo zinazowekwa haziumizi upande wowote.

Kwa mujibu wa wadau hao, utaratibu huo mpya unapaswa kuwa rafiki kwa wadau wote na kusaidia kuongeza ufanisi wa shughuli za bandari bila kuongeza mzigo kwa wafanyabiashara na wananchi.

Katika hatua nyingine,  Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha TACAS Ephraim Mwankusye ameiomba Serikali kuzingatia kikamilifu matakwa ya GN (Tangazo la Serikali) inayohusu uendeshaji wa shughuli za bandari, wakisisitiza kuwa kazi zinazopaswa kufanywa na wazawa zisifanywe na wageni.

Amesems utekelezaji huo utasaidia kuhakikisha Watanzania wananufaika ipasavyo na fursa zinazotokana na shughuli za bandari pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa


 

0/Post a Comment/Comments