TRA YAANZA KUCHUKUA HATUA UTARATIBU MPYA UINGIZAJI MAFUTA YA KULA

******

KAMISHINA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) Yusuph Mwenda amesema Mamlaka hiyo tayari imeanza kuchukua hatua kuelekea kuanza kutumika kwa utaratibu mpya wa kuingiza mafuta ya kula Tanzania Bara kutoka Zanzibar. 

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Machi 24.2026 jijini Dar es Salaam Mwenda amesema miongoni mwa hatua zilizoanza kuchukuliwa ni pamoja na kuunda kamati ndogo ya wataalam inayohusisha Wizara ya Kilimo kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko, maofisa wa Forodha na waagizaji wa mafuta kwaajili ya kuweka utaratibu utakaoanza kutumika kuingiza mafuta hayo hivi karibuni.

Amesema utaratibu huo mpya unalenga kuwezesha biashara ya Mafuta baina ya Tanzania Bara na Zanzibar na kuchangamsha biashara katika Bandari za Bagamoyo, Mbweni na Kunduchi ambazo ndiyo hutumika kuingiza mafuta hayo.

"Tutatoa punguzo kwa mafuta yanayoingia Tanzania Bara kutoka Zanzibar ili kuwawezesha wanaoingiza mafuta hayo kupata faida, Serikali kupata kodi na pia kulinda viwanda vya ndani" amesema Mwenda.

Aidha Kamishna Mwenda amewaonya wafanyabiashara wa bidhaa hiyo watakaojihusisha na magendo baada ya kuanza kutumika kwa utaratibu huo kuwa Serikali haitasita kuwachukuli hatua kwa mujibu wa sheria. 

Katika hatua nyingine Kamishna Mkuu amesema TRA itaendelea kutoa elimu ya kodi kwa wananchi wote na kuwezesha biashara baina ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi analipa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Mhe. Ali Suleiman Ameir imeipongeza TRA kwa uwajibikaji na kuahidi kuwa wataendelea kushirikiana nayo katika kuieleza jamii umuhimu wa kulipa kodi.

Akizungumza katika kikao hicho, Ameir kazi inayofanywa na TRA imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa hususan kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo hatua ambayo kwa kiasi kikubwa inachochea ukuaji wa uchumi.

Aidha amesema wamefanya ziara hiyo mahususi kwaajili ya kujifunza namna mfumo wa usimamizi wa kodi za ndani (IDRAS) unavyofanya kazi na kuipongeza TRA kwa kuanza kutumia mfumo huo ambao umeweza kuokoa muda wa walipakodi kwa kupata huduma popote walipo huku ukipunguza kwa kiasi kikubwa watumishi wa TRA kuonana na Walipakodi. 

Wajumbe wengine wa Kamati ya Bunge ya Baraza la wawakilishi waliohudhuria kikao hicho wamepongeza juhudi za udhibiti wa magendo zinazofanywa na TRA huku wakiahidi kusimamia vizuri matumizi ya kodi zinazokusaywa.





0/Post a Comment/Comments