MADIWANI MAKANGARAWE WASHIRIKIANA NA UWT KUSAIDIA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM

Diwani wa Kata ya Makangarawe Fadhili Mboga akizungumza katika hafla ya utoaji wa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wenye uhitaji kwenye shule ya msingi Yombo Dovya Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam  leo tar 6/3/2026
Diwani wa Viti Maalum, Farida Saumu Mkwanywe akizungumza katika hafla ya utoaji wa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wenye uhitaji kwenye shule ya msingi Yombo Dovya Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam leo tar 6/3/2026
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Yombo Dovya Salum Gawaza  akizungumza katika hafla ya utoaji wa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wenye uhitaji kwenye shule ya msingi Yombo Dovya Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam leo tar 6/3/2026

Picha ya pamoja ya viongozi wakati wa hafla ya utoaji wa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wenye uhitaji kwenye shule ya msingi Yombo Dovya Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam leo tar 6/3/2026 (picha zote na Mussa Khalid)
.......................

Na Hawa Ismail- Dar es Salaam 

Diwani wa Viti Maalum, Farida Saumu Mkwanywe, na Diwani wa Kata ya Makangarawe, Fadhili Mboga, wameungana na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Makangarawe kutoa msaada kwa watoto wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Yombo Dovya, iliyopo wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam. 

Msaada huo umetolewa Machi 6, 2026 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambayo kilele chake hufanyika kila mwaka Machi 8. Madiwani hao walisema tukio hilo linaonyesha upendo na mshikamano kwa watoto wenye mahitaji maalum katika jamii. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Diwani wa Viti Maalum Farida Saumu Mkwanywe aliipongeza UWT Makangarawe kwa kuonesha moyo wa huruma kwa kuwasaidia watoto hao na kuwapa furaha. 

“Nawapongeza sana Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Makangarawe kwa kuonesha moyo wa upendo kwa kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Yombo Dovya. Sisi kama viongozi tutaendelea kuwaunga mkono katika juhudi hizi za kijamii,” alisema Mkwanywe.

Kwa upande wake, Katibu wa UWT Makangarawe, Salma Lupinga, alisema kuwa katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu waliamua kutembelea watoto wenye mahitaji maalum ili kushirikiana nao na kuwapa msaada pamoja na walimu wanaowalea.

Alisema UWT Makangarawe imekuwa ikifanya shughuli mbalimbali za kijamii kila mwaka, na safari hii waliona ni vyema kusherehekea siku hiyo kwa kuonesha upendo kwa watoto hao pamoja na walimu wao.

Naye Diwani wa Kata ya Makangarawe, Fadhili Mboga, aliwapongeza wanawake wa UWT Makangarawe kwa maono yao ya kusaidia jamii na kuwashukuru walimu wanaowalea watoto hao kwa kujitolea kuwasaidia hadi kufikia hatua ya kuendelea na masomo ya sekondari na hata vyuo vya ufundi.

Mboga alisisitiza kuwa wanawake ni nguvu kubwa katika jamii, akitolea mfano kuwa katika sekta mbalimbali za jamii, ikiwemo elimu na shughuli za kijamii, wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma na mchango mkubwa kwa maendeleo ya jamii. 

Aidha, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Yombo Dovya alisema kituo hicho kina watoto 100 wenye mahitaji maalum, wakiwemo wavulana 67 na wasichana 33. Alifafanua kuwa watoto hao wamegawanywa katika hatua tatu za kujifunza, huku wakifundishwa zaidi stadi za maisha zinazowawezesha baadhi yao kuendelea na masomo katika vyuo vya ufundi stadi (VETA). 

Kwa upande wake, mwalimu mlezi wa watoto wenye ulemavu, Bi. Naghenywa Mshighati, aliwashukuru madiwani pamoja na wanawake wa Makangarawe kwa kuwatembelea na kuwapa zawadi watoto hao, akisema kitendo hicho kinaonesha wazi jinsi wanawake walivyo jeshi kubwa katika kuonesha upendo na kujali jamii.


 

0/Post a Comment/Comments