Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Bw. Gwalusajo Kapande amesema kuwa utekelezaji wa mradi wa Uendelezaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) katika Manispaa hiyo utaleta mabadiliko chanya kwa wana Mpanda na wageni katika utoaji huduma na mahitaji mbalimbali ya usafiri na usafirishaji, mazingira bora ya shughuli za kiuchumi na ongezeko la mapato kwa Halmashauri.
Hayo ameyasema katika mahojiano maalum ambapo amebainisha kuwa ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 8.49 katikati ya mji zitasaidia katika shughuli za biashara na kijamii na mara mradi utakapokamilika mji wa Mpanda utapendeza na maeneo mengi yatafikika kwa urahisi kipindi chote cha mwaka.
"Barabara hizi zitapendezesha mji wetu wa Mpanda sambamba na kuinuka kwa uchumi kwani tutapata wawekezaji wengi kutokana na uwepo wa barabara nzuri hapa mjini. Jukumu letu ni kuitunza miundombinu hii itakayojengwa kwa gharama kubwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu,” amesisitiza.
Naye, Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mhe. Charles Philipo amesema kuwa matarajio ya wanampanda ni kukamilika kwa mradi huo wa ujenzi wa barabara kwa wakati na kuongeza tija katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwani maeneo mengi ya mji yatafikika kwa urahisi.
"Mradi huu utabadilisha maisha ya wakazi wa Mpanda, tunaishukuru serikali kwa uamzi huu wa kuleta mradi muhimu katika mji wetu kwani sasa tutaanza kupata wawekezaji baada ya kukamilika kwa mradi huu na maisha ya watu yatakuwa yameboreshwa", amesema Mhe. Charles.
Akitoa pongezi kwa niaba ya wananchi, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Mhe. Haidary Hemed Sumry amesema kuwa licha ya mradi huo kutarajiwa kuboresha huduma za kijamii, pia utasaidia katika sekta ya biashara kwani maeneo mengi yatafikika kwa urahisi.
Akitoa maelezo kuhusu mradi huo, Mratibu wa mradi ambaye pia ni Meneja wa TARURA wilaya ya Mpanda, Mhandisi Kahoza Joseph amezitaja barabara zitakazojengwa na mradi ni pamoja na barabara ya Mkumbo Junction –Nsemulwa Health Center (Km 1.68), barabara ya Nsemulwa Health Center – Sokoine (Km 1.23) na barabara ya Kapufi (mita 760)na barabara ya Sumry (mita 460)
Aidha, barabara nyingine zinazojengwa na Mradi huo ni barabara ya Pinda (mita 270), barabara ya Fimbo ya Mnyonge (mita 390), barabara ya Fish Market (mita 330), barabara ya Mpanda Hotel (mita 760), barabara ya Mikocheni Junction – White Gireffe (km 1.88) na barabara ya Homeground (mita 730).
Ameeleza kuwa mradi huo kwa manispaa ya Mpanda ulianza tarehe 2/1/2026 na unatarajia kukamilika ifikapo tarehe 31/3/2027 na utagharimu Shilingi Bilioni 21.9.
Naye, mkazi wa Mpanda Bw. Gaudence Kinyonto ameipongeza Serikali kwa kuleta mradi utakaoboresha barabara za ndani ya mji wa Mpanda na kuwezesha maeneo mengi ya mji huo kufikika kwa urahisi.
Lengo kuu la mradi wa TACTIC ni kuboresha usimamizi wa ukuaji wa miji pamoja na kuziwezesha Halmashauri za Miji na Majiji kutoa huduma bora kwa wananchi.





Post a Comment