Dar es Salaam, Machi 20, 2026
Wananchi nchini wametakiwa kujenga utamaduni wa kuchambua taka ngumu majumbani na katika maeneo yao ya kazi, badala ya kuzitupa ovyo, ili kulinda mazingira na kuongeza thamani ya taka hizo kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Balozi wa Mazingira wa kujitolea nchini, Moses Mwakibolwa, wakati akizungumza kuelekea maadhimisho ya Siku ya Taka Sifuri Duniani yanayotarajiwa kufanyika tarehe 30 Machi 2026.
Amesema kuchambua taka ni hatua muhimu inayoweza kusaidia katika urejelezaji na matumizi ya taka kama nishati mbadala, hali itakayochangia kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuongeza fursa za kiuchumi.
“Mabaki ya vyakula yanaweza kutumika kama mbolea ya asili au chakula cha mifugo kama kuku. Hivyo, badala ya kuwa mzigo, taka zinaweza kuwa rasilimali yenye manufaa makubwa,” amesema Mwakibolwa.
Aidha, amesisitiza kuwa sekta ya usimamizi na urejelezaji taka ina uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira kwa vijana, akiwahimiza kuanzisha vikundi vya mazingira vitakavyoshughulika na ukusanyaji na uchakataji wa taka.
Katika hatua nyingine, Mwakibolwa ameeleza kuwa baada ya maadhimisho ya Siku ya Taka Sifuri, wananchi wameombwa kushiriki katika darasa maalum la mazingira litakalofanyika tarehe 04 Aprili 2026 katika Kata ya Bunju, eneo la Boko CCM, Shule ya Msingi Boko.
Amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuhudhuria mafunzo hayo ili kujifunza zaidi kuhusu utunzaji wa mazingira na usimamizi sahihi wa taka, akibainisha kuwa wataalamu kutoka serikalini wanatarajiwa kushiriki na kutoa elimu kwa wananchi.
“Nawaomba wananchi msikose kufika katika darasa hili muhimu, kwani litatoa maarifa yatakayosaidia kuboresha maisha yetu na kulinda mazingira yetu,” ameongeza Mwakibolwa.
Maadhimisho ya Siku ya Taka Sifuri Duniani hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha matumizi bora ya rasilimali na kupunguza uzalishaji wa taka, sambamba na kulinda mazingira kwa maendeleo endelevu
.jpeg)
Post a Comment