WANAWAKE WA TCAA WATOA MSAADA GEREZA LA SEGEREA KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA WANAWAKE

::::::
Kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, wanawake kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wametembelea Gereza la Segerea jijini Dar es Salaam Machi 06, 2026 na kutoa msaada wa vifaa na mahitaji mbalimbali kwa ajili ya kuwafariji wafungwa wanawake na watoto wanaoishi gerezani hapo.

Katika ziara hiyo, wanawake hao walikabidhi mahitaji muhimu kwa uongozi wa gereza ikiwemo vyakula, mavazi, taulo za kike, maziwa ya watoto pamoja na vifaa vya usafi, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za kuboresha ustawi wa wafungwa wanawake na watoto waliopo gerezani.

Akizungumza kwa  niaba ya Menejimenti ya TCAA, Afisa Rasilimali Mkuu, Bi. Grace Kiunsi, alisema hatua hiyo ni sehemu ya utamaduni wa Mamlaka kushiriki katika shughuli za kijamii na kuendelea kuunga mkono makundi yenye uhitaji maalum katika jamii.

Alisema TCAA inaamini kuwa kuwatia moyo na kuwasaidia wanawake walioko katika mazingira mbalimbali ni sehemu ya kuchangia ujenzi wa jamii yenye mshikamano, utu na kujali.

Kwa upande wa Gereza akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Gereza, Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Ngajebule Mbuguru, aliishukuru TCAA kwa msaada huo akibainisha kuwa unaleta faraja kwa wafungwa na kuwakumbusha kuwa bado ni sehemu ya jamii inayowajali.

Aliongeza kuwa vifaa na mahitaji yaliyotolewa vitasaidia kukidhi baadhi ya mahitaji muhimu ya kila siku ya wafungwa wanawake na watoto waliopo gerezani, huku Jeshi la Magereza likiendelea kutoa mafunzo ya ujuzi mbalimbali kwa wafungwa ili kuwaandaa kujitegemea pindi watakaporejea katika jamii.

Hatua hiyo imetajwa kuwa mchango muhimu katika kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuendeleza jamii yenye usawa na huruma kwa wote, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake.




 

 

0/Post a Comment/Comments