BODI MPYA YA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YAANZA NA MAJUKUMU MAZITO DODOMA

..........

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameielekeza Bodi mpya ya Wadhamini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa kuhakikisha inasimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi yote iliyoanzishwa na bodi zilizopita pamoja na kubuni miradi mipya itakayoboresha huduma za afya kwa wananchi.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Bodi ya pili ya wadhamini wa hospitali hiyo, Mhe. Mchengerwa amesema ni muhimu kwa bodi hiyo kufanya vikao vya mara kwa mara ili kutatua changamoto kwa wakati na kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.

Amesisitiza kuwa hospitali hiyo inatarajiwa kuwa ya kipekee kitaifa, hivyo ni wajibu wa bodi kuhakikisha inaendelea kutoa huduma bora zinazokidhi mahitaji ya wananchi sambamba na kuanzisha huduma na miradi mipya.

“Tunataka kuona huduma zote muhimu, ikiwemo za kifedha, zikifanyika hapa Dodoma. Aidha, dhamira ya kuifanya hospitali hii kuwa ya Taifa inaungwa mkono kwa kuwa ipo katika makao makuu ya nchi,” amesema.

Waziri huyo amewataka wajumbe wa bodi kutumia utaalamu wao kusimamia kwa ufanisi maendeleo ya hospitali hiyo na kuendeleza misingi ya utendaji bora, akibainisha kuwa bodi iliyopita ilifanya kazi kubwa katika kipindi cha kuanzisha huduma rasmi za matibabu.

Ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa mradi wa uzalishaji wa hewa tiba (oxygen) pamoja na Kituo cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Benjamin Mkapa, ambacho kwa sasa kinadahili wanafunzi 270 kwa mwaka katika fani mbalimbali za afya.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema serikali inatambua mchango wa watumishi wa sekta ya afya na kuwataka kuendelea kujitoa kikamilifu katika kuwahudumia Watanzania, akisisitiza umuhimu wa kubadili mitazamo na kufanya kazi kwa bidii ili kufikia maendeleo ya sekta hiyo.

“Ninachowaomba ni kuendeleza wito wa kufanya kazi kwa bidii tuliokabidhiwa na waasisi wa taifa hili. Tunapaswa kutumia utaalamu wetu kuokoa maisha ya Watanzania,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dkt. Edward Hosea, amesema hospitali hiyo imepokea gari la kliniki tembezi (mobile clinic van) lililotolewa na mradi wa East Africa Comprehensive Women Center Project, kwa ajili ya kusaidia uchunguzi wa saratani kwa wanawake katika maeneo ya pembezoni.

Amesema hatua hiyo itaongeza ufanisi wa utoaji huduma, hususan kwa wananchi wanaoishi mbali na hospitali hiyo.

Hata hivyo, Dkt. Hosea ameeleza changamoto zinazoikabili hospitali hiyo, ikiwemo upungufu wa watumishi 444, uhaba wa magari ya kutolea huduma pamoja na deni la shilingi bilioni 14.39 linalodaiwa kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

Ameeleza kuwa kupatikana kwa fedha hizo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha utoaji wa huduma na kutatua changamoto zilizopo.

Uzinduzi wa bodi hiyo unakuja baada ya bodi iliyopita kumaliza muda wake, huku ikisifiwa kwa juhudi zake za kuanzisha na kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo ya hospitali hiyo.





 

0/Post a Comment/Comments