DHAMIRA YA SERIKALI YADHIHIRIKA; LANGO MAMIRE LAANZA KUPOKEA WATALII - TARANGIRE

........

Na. Jacob Kasiri - Tarangire.

Dhamira ya serikali ya kukuza utalii na kufikisha watalii milioni nane (08) ifikapo 2030 sasa inaonekana kwa vitendo, baada ya lango la Mamire lililopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Tarangire kukamilika na leo Aprili 23, 2026, lango hilo limepokea mgeni mmoja kutoka Taifa la Australia.

Hatua hii inafungua ukurasa mpya wa kiuchumi kwa jamii zinazozunguka hifadhi hiyo huku ikichagiza katika kukuza mapato, ajira na kuibua fursa za utalii wa kiutamaduni kwa mkoa wa Manyara hasa katika mji wa Babati.

Akikata (permit) kibali cha kuingia ndani ya Hifadhi ya Taifa Tarangire kupitia katika lango hilo jipya, Bi. Cindy Snart alisema kuwa amefurahishwa na hatua ya TANAPA kufungua lango hilo, na hii itawarahisishia na kuwapunguzia watalii wengi mwendo kwa kutokea Babati mjini hadi lango la Mamire ambalo ni kilometa 21 tu.

Naye, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Tarangire Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Tutindaga George aliwasihi na kuwahimiza wenye Makapuni ya utalii na usafirishaji kutumia lango hilo kwani limekamilika na huduma zote za msingi zinazohitajika na watalii ziko vizuri ikiwemo maeneo ya kupumzikia (Vimbweta).

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Kaskazini Dkt. Beatrice Kessy alisema kuwa kukamilika kwa lango la Mamire kunaifanya Hifadhi ya Taifa Tarangire kuwa na maeneo matano ya kuingilia wageni, kitu kitakachoongeza mtawanyiko wa wageni katika maeneo tofauti.

Aidha, Kamishna Kessy aliongeza; “Lango la Mamire ni kubwa na linauwezo wa kuhudumia watalii zaidi ya 2000 kwani lina madirisha mengi ya kutolea huduma, kadri wageni watakavyoongezeka ndivyo na vyumba vya kutolea huduma vitaendelea kuongezewa vitendea kazi.”

Diwani wa Kata ya Mamire Mhe. Augustino Sosiya alisema kuwa lango hilo licha ya kuingiza watalii, tayari wananchi wake watano wameshapata ajira, na amewasihi wawekezaji kuja kuwekeza katika malazi na vyakula katika Kata hiyo ambayo ni mnufaika namba moja wa mradi huo.

Mradi wa lango la Mamire umegharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 3.9 ikihusisha lango lenye (Smart Gate), majengo matano kwa ajili ya malazi kwa maafisa na askari, eneo la maegesho ya magari zaidi 98, Kisima cha maji, Majengo mawili ya vyoo wakati wa kuingia na kutoka, mifumo ya TEHAMA, Vimbweta vya mapumziko wakati wa kuingia na kutoka, “Generator kwa ajili ya standby” na umeme wa gridi ya Taifa (TANESCO).


 

0/Post a Comment/Comments