........
Na Carlos Claudio, Dodoma.
UONGOZI wa Shule ya Sekondari Efforts iliyopo Ukuni, Bagamoyo mkoani Pwani, umesema ziara ya masomo waliyoifanya katika Kituo cha Michoro ya Miambani Kondoa imelenga kuwapatia wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo na kupanua uelewa wao katika nyanja mbalimbali za kitaaluma.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Shule hiyo, Hussein Mussa, alisema lengo kuu ni kuwajengea wanafunzi uelewa mpana kuhusu masuala ya ufundi, historia na taaluma mbalimbali zinazotolewa katika taasisi za elimu ya juu.
Alisema kupitia ziara hiyo, wanafunzi wameweza kuona kwa vitendo fursa zilizopo katika sekta tofauti, jambo litakalowasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kitaaluma wanapohitimu masomo yao ya sekondari.
“Ni muhimu kwa wanafunzi kupata uzoefu wa vitendo ili waweze kuelewa kwa undani wanachojifunza darasani na hivyo kuchagua mwelekeo sahihi wa maisha yao ya baadaye,” alisema Mussa.
Katika ziara hiyo, wanafunzi walipokelewa na waongozaji watalii katika kituo hicho cha michoro ya miambani na kupewa elimu ya kihistoria kuhusu urithi wa taifa, kabla ya kutembezwa na kujionea michoro mbalimbali yenye thamani kubwa ya kiutamaduni na kihistoria.
Mbali na hilo, wanafunzi hao walipata fursa ya kusafiri kwa treni ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), ambapo walijionea maendeleo ya miundombinu ya usafiri nchini.
Ziara hiyo pia iliwapeleka katika Mji wa Kiserikali Mtumba, VETA pamoja na Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) , ambako walijifunza namna taasisi hizo zinavyofanya kazi na mchango wake katika maendeleo ya taifa.
Baada ya kukamilika kwa ziara hiyo, wanafunzi walieleza kuvutiwa na mambo mbalimbali waliyoyaona, wakisema yamewapa hamasa mpya ya kusoma kwa bidii ili kufikia ndoto zao.
Aidha, waliipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika miundombinu na sekta ya elimu, wakieleza kuwa hatua hiyo ina mchango mkubwa katika kukuza maendeleo ya vijana na taifa kwa ujumla.










Post a Comment