Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2026/27, leo, tarehe 22 Aprili 2026, Bunge jijini Dodoma.
..
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imekagua jumla ya vituo 672 vya mafuta kote nchini katika jitihada za kuimarisha udhibiti wa ubora wa mafuta na kulinda maslahi ya watumiaji.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 22,2026 bungeni Dodoma.
Katika ukaguzi huo, vituo 50 sawa na asilimia 7.44 vilibainika kuuza mafuta yasiyokidhi viwango vilivyowekwa, hatua iliyochochea mamlaka hiyo kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika. Hatua hizo zilijumuisha kufungiwa kwa vituo husika, kutozwa faini pamoja na kuwasilishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kulipa kodi walizokwepa.
Mbali na ukaguzi wa ubora, EWURA pia ilifanya operesheni maalum ya kufuatilia mwenendo wa usambazaji wa mafuta, ambapo ilibaini vituo vitatu vilivyokuwa vimeficha mafuta kwa makusudi vikisubiri mabadiliko ya bei. Serikali ilichukua hatua za haraka kwa kuvifungia vituo hivyo na kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Hata hivyo amesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya mafuta nchini kupitia utekelezaji wa programu ya uwekaji vinasaba kwenye mafuta, hatua inayolenga kudhibiti ubora wa bidhaa hiyo pamoja na kuhakikisha ukusanyaji sahihi wa mapato ya kodi.
Amesema Kupitia EWURA utekelezaji wa mpango huo umeonesha mafanikio makubwa kufikia Machi 2026, ambapo jumla ya lita bilioni 1.51 za petroli na lita bilioni 2.02 za dizeli ziliwekewa vinasaba. Kiasi hicho kinaonesha ongezeko la asilimia 14 kwa petroli na asilimia 10 kwa dizeli ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2024/25.
Hata hivyo, kwa upande wa mafuta ya taa, kiasi kilichowekewa vinasaba kilifikia lita milioni 2.80, ikiwa ni pungufu la asilimia 40, hali inayotafsiriwa kuwa na mabadiliko ya mwenendo wa matumizi au usambazaji wa bidhaa hiyo sokoni.
Hatua hizi zinaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha sekta ya mafuta inasimamiwa kwa uwazi na ufanisi, huku ikihakikisha haki kwa watumiaji na kuongeza mapato ya Taifa. Aidha, juhudi hizo zinasaidia kudhibiti vitendo vya udanganyifu vinavyoweza kuhatarisha uchumi na ustawi wa wananchi.
Post a Comment