Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2026/27, leo, tarehe 22 Aprili 2026, Bunge jijini Dodoma.
....
Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeendelea kuimarisha usimamizi na udhibiti wa shughuli za bidhaa za mafuta ya petroli nchini, hatua inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa nishati, usalama wa miundombinu pamoja na ubora wa huduma kwa wananchi.Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 22,2026 bungeni Dodoma.
Akieleza mafanikio ya utekelezaji huo hadi Machi 2026, EWURA imefanikiwa kutoa jumla ya leseni 636 kwa biashara mbalimbali katika sekta ndogo ya mafuta na gesi. Leseni hizo zinahusisha vituo vya mafuta mijini na vijijini, maghala ya kuhifadhia mafuta, pamoja na biashara ya usambazaji na uuzaji wa gesi ya kupikia (LPG) na vilainishi.
"Takwimu zinaonesha kuwa vituo vya mafuta mijini vimeongoza kwa kupata leseni nyingi zaidi, huku pia juhudi zikielekezwa katika maeneo ya vijijini ili kupanua huduma na kuongeza upatikanaji wa nishati kwa wananchi wa maeneo hayo. Hatua hii inaakisi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha huduma za mafuta zinawafikia wananchi wote bila kujali maeneo yao."amesema Mhe.Ndejembi
Katika kuimarisha miundombinu ya sekta hiyo, EWURA pia ilitoa vibali 288 vya ujenzi wa miundombinu ya mafuta, ambapo vibali 137 vilihusu maeneo ya mijini na 143 vijijini. Vibali vingine vilihusisha maghala ya kuhifadhi mafuta na gesi, pamoja na miundombinu ya matumizi ya viwandani na migodini.
Sambamba na utoaji wa leseni na vibali, EWURA imeendelea kusimamia kwa karibu taratibu za uagizaji na usambazaji wa mafuta nchini. Katika ukaguzi wa ubora wa bidhaa, jumla ya sampuli 648 zilipimwa, ambapo sampuli 608 sawa na asilimia 93.83 zilikidhi viwango vinavyotakiwa. Vituo 22 vilivyobainika kuuza mafuta yasiyokidhi viwango vilichukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufungiwa na kutozwa faini.
Aidha, ukaguzi wa miundombinu ya mafuta ulifanyika katika vituo 544, ambapo asilimia 86.95 ya miundombinu hiyo ilikidhi viwango vya ubora, ikiwa ni pamoja na masuala ya afya, usalama na mazingira. Wamiliki wa vituo 95 ambavyo havikukidhi vigezo walielekezwa kufanya maboresho ili kuendana na viwango vilivyowekwa.
Kwa ujumla, hatua hizi zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha sekta ya mafuta inakuwa salama, yenye ufanisi na inachangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa, huku ikilinda maslahi ya watumiaji na mazingira.
Post a Comment