NA: MWANDISHI WETU, PANGANI
Katika kuhakikisha ari ya wanafunzi kusoma inaongezeka na kuongeza ufaulu wa shule, uongozi wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga, imetoa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri kawa kupata Daraja la Kwanza katika Mitihani ya Robo Muhula wa Kwanza kwa mwaka 2026
Tukio la kukabidhi zawadi hizo, limefanyika Aprili 30, 2026, shuleni hapo ambapo wito umetolewa kwa wanafunzi kusoma kwa bidii ili waweze kufaulu vizuri mitihani yao huku uongozi wa shule ukiahidi kuendelea kuwatambua wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani mbalimbali kwa kuwapa motisha.
Katika tukio hilo, Makamu Mkuu wa Shule, Masoud Abdallah, amesema wanafunzi wanapaswa kusoma kwa bidii ili kuweza kufikia ndoto zao za kimaisha kwani elimu ndiyo nyenzo ya kufikia malengo yao.
"Leo tunatoa zawadi kwa wanafunzi waliopata Daraja la Kwanza (Division One) kuanzia Kidato cha Kwanza Hadi Cha Nne, hii iwe chachu kwa wengine kusoma kwa bidii, malengo ya shule yetu ni kuhakikisha wanafunzi wote wanafaulu ili waweze kuendelea na masomo," amesema Masoud.
Mwalimu wa Taaluma wa shule hiyo, Chiku Iddy amesema wanafunzi wanapaswa kuongeza kasi ya ujifunzaji kwani dunia ya leo inahitaji watu wenye maarifa na ujuzi.
Katika hatua nyingine, Mwalimu wa Michezo wa shule hiyo, Isihaka Shekalaghe amewaasa wanafunzi kusoma kwa bidii na wajiepushe na mahusiano ya kimapenzi kwani yanachangia kushusha ufaulu wa masomo.








Post a Comment