Na: Mwandishi Wetu, Dar
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imefanikiwa kuvuka malengo yake ya makusanyo kutoka kwa wanufaika wa mikopo hiyo katika kipindi cha miezi mitatu Januari hadi Machi, 2026, hali inayoongeza fursa ya waombaji wa mikopo hilo kuongezeka.
Kwa mujibu wa taarifa ya HESLB, makusanyo yameongezeka kutoka kwa wanufaika wake, jambo linaloleta faraja kwa taasisi hiyo.
"Miezi mitatu ya Januari hadi Machi, Bodi ililenga kukusanya shilingi bilioni 18.3 kwa kila mwezi, lakini mwezi Januari zimekusanywa shilingi bilioni 20.4, mwezi Februari bilioni 19.4 na mwezi Machi bilioni 20.9," imeeleza taarifa hiyo.
Mafanikio ya makusanyo hayo yametokana wa mwamko wa wanufaika wa mikopo ya elimu kuanza kulipa mikopo yao kwa hiari, baada ya kuhitimu na kuwa na vipato kwa kuajiriwa au kujiajiri wenyewe.
Vilevile, waajiri kutoa taarifa za wanufaika pindi wanapoanza kazi katika taasisi wanazozisimamia, jambo linaloiwezesha Bodi kuongeza makusanyo yake.
Sanjari na hilo, kuimarisha kwa mifumo ya kiteknolojia ambapo sasa mifumo inasomana, imesaidia sana kuongeza makusanyo kutoka kwa wanufaika.
Takwimu zinaonyesha wanufaika 539,103 ambao mikopo yao imeiva wamekopeshwa jumla ya shilingi trilioni 2.76, katika fedha hizo, Bodi imefanikiwa kukusanya trilioni 1.84 kutoka kwa wanufaika 403,917 ambao wameanza kurejesha mikopo yao huku wanufaika 135,186 waliokopeshwa bilioni 920 wakiwa bado hawajaanza kurejesha mikopo yao.
Pia, katika mwaka wa fedha 2025/2026, kwa miezi tisa, Bodi imefanikiwa kukusanya bilioni 175.9 sawa na asilimia 106.6 ya lengo la kukusanya bilioni 165 kwa miezi hiyo.
Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, lengo la makusanyo ya mwaka ni kufikisha shilingi bilioni 220.3, kutokana na mwenendo uliopo wa makusanyo, Bodi inatarajiwa kuvuka lengo na kukusanya bilioni 225 ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha yaani Juni 30, 2026.

Post a Comment