HILDA NEWTON AITWA POLISI "MADAI YA LISSU KUTAKA KUUWAWA NA SERIKALI"

Jeshi la Polisi Nchini Tanzania leo Jumatano Aprili 22, 2026 limemtaka Mwanasiasa Hilda Newton kuripoti kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Jijini Dar Es Salaam ili kuwasilisha ushahidi wa tuhuma alizozichapisha na kusambaza katika Mitandao ya Kijamii Nchini kuwa Serikali imepanga kumuua Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Bw. Tundu Lissu.

Wito huo umekuja kufuatia uchunguzi wa taarifa aliyoichapisha Hilda mnamo Aprili 10, 2026, ikidai kuwa kuna njama za kumuua kiongozi huyo kwa risasi. Polisi wamebainisha kuwa, kwa kuwa mhusika alishatangaza kuwa ana ushahidi wa madai hayo, ni lazima auwasilishe mbele ya wapelelezi ili kukamilisha taratibu za kisheria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Hilda Newton anapaswa kufika katika jengo la Makao Makuu Ndogo ya Polisi, Mtaa wa Ohio, tarehe 24 Aprili 2026 saa nne asubuhi.


Upelelezi huu unaendeshwa chini ya kifungu cha 11 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2023, ambacho kinawapa polisi mamlaka ya kumsaili mtu yeyote mwenye taarifa za jinai. Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa linaendelea na ukusanyaji wa ushahidi ili kubaini ukweli wa taarifa hizo ambazo zimezua taharuki kwa umma.

"lli kukamilisha uchunguzi, Jeshi la Polisi linamwelekeza Hilda Newton afike katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai iliyopo katika Jengo la Makao Makuu Ndogo ya Polisi iliyopo Mtaa wa Ohio Jijini Dar es Salaam tarehe 24.4.2026 saa nne (4) asubuhi ili aweze kuwasilisha ushahidi aliyosema na kutangazia umma kuwa anao. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 11 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa yaJinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2023."


 

0/Post a Comment/Comments