Kampeni "Kiduchu Fresh Tunasonga" na uendelevu wa utoaji mikopo ya elimu

...............

Na: Dk. Reubeni Lumbagala

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ina jukumu la kutoa mikopo kwa waombaji ili waweze kutimiza malengo yao ya kupata elimu katika taasisi mbalimbali za elimu kama vyuo vya kati na vyuo vikuu. 

Pia, HESLB inawajibika kukusanya mikopo kutoa kwa wanufaika wake ili kuwezesha waombaji wengine waweze kupata mikopo ili nao waweze kupata elimu. Kwa zaidi ya miaka 20 sasa, serikali kupitia HESLB, imewezesha vijana wengi wa Kitanzania kutimiza malengo yao ya kielimu kwa kuwakopesha mikopo ya elimu.

Wengi wa vijana hao ni wale wanaotoka familia zenye changamoto za kiuchumi ambazo pengine bila kuwezeshwa mikopo, wasingeweza kumudu kupata elimu kutokana na gharama kubwa za elimu zilivyo huko vyuoni. Hii ndiyo kusema, baadhi yao wasingeweza kutimiza ndoto zao za kusoma fani na taaluma mbalimbali kama wasingepata mkopo wa elimu.

Kwa kuwa tayari fedha nyingi zimewekezwa kwa kukopesha vijana wengi, HESLB inayo kazi kubwa ya kukusanya mikopo hiyo kutoka kwa wanufaika wake hasa waliohitimu masomo na kuwa na kipato katika sekta rasmi au isiyo rasmi.

Kwa wanufaika ambao wameajiriwa serikalini au sekta binafsi kumekuwa na urahisi wa kuwapata kutokana na waajiri kutuma taarifa za wafanyakazi wao kwa HESLB ili waweze kukatwa asilimia 15 ya mshahara kwa mujibu wa sheria.

Lakini kwa wanufaika ambao wamejiajiri wenyewe kama mama na baba lishe, bodaboda, wamachinga, mafundi wa fani mbalimbali, wajasiriamali, kumekuwa na ugumu wa kuwapata, kwani wao wanapaswa kujitokeza wenyewe ili kuanza kurejesha mikopo yao kwa hiari, lakini ukimya wa baadhi yao unasababisha HESLB kukosa marejesho kutoka kwao.

Baadhi ya wahitimu wana mtazamo kuwa ni mpaka waajiriwe na serikali au katika sekta binafsi, ndipo wanapaswa kuanza kurejesha mikopo yao, yaani wanadhani ni mpaka wawe na mshahara ndipo waanze kulipa.

Iko hivi: Muhimu ni kuwa na kipato tu, iwe ni kuajiriwa au kujiajiri, mnufaika mhitimu anapaswa aanze kulipa ili waombaji mikopo wengine wenye sifa nao wakopeshwe kama wao walivyokopeshwa walipokuwa wanafunzi vyuoni enzi hizo.

HESLB ina malengo ya kujijenga katika namna ambayo kutakuwa na uendelevu wa utoaji wa mikopo yaani wakopeshe wanafunzi, lakini wanafunzi hao wanapohitimu na kuwa na kipato, waanze kurejesha mikopo hiyo ili wengine nao wakopeshwe.

Mnamo Aprili 17, 2026, katika ofisi za HESLB, Kanda ya Mashariki, Jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, alizindua kampeni maalum ya kuhamasisha wanufaika hasa waliojiajiri wenyewe kuanza kulipa mikopo yao ya elimu.

Kampeni hiyo ijulikanayo kwa jina la "Kiduchu Fresh Tunasonga," inahamasisha mnufaika mhitimu mwenye kipato kidogo kuwa anaweza kuanza kurejesha mkopo wake ulioiva kwa kuanza na kiasi cha shilingi 5,000 na kuendelea, ili hata yule mwenye kipato kidogo sana aweze kumudu kiwango hicho rafiki.

Katika hotuba yake, Naibu Waziri Wanu amewasihi wanufaika waanze kulipa mikopo yao kidogo kidogo ndiyo maana Bodi imeweka kiwango hicho kidogo ili wengi waweze kumudu.

"Kiduchu ni kidogo ya kidogo … na upekee wake ni kuwafikia wanufaika wengi wenye kipato cha chini ili waweze kurejesha mikopo yao kulingana na uwezo wao, msisubiri hadi muwe na fedha nyingi, anzeni na kiduchu mlichonacho leo. Kila mchango hata uwe mdogo kiasi gani, una mchango mkubwa katika kujenga Taifa letu," alisema Wanu.

Takwimu zinaonesha kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2025/2026, serikali imeshatoa shilingi trilioni 3.6 kwa wanafunzi mbalimbali.

Lengo la kampeni ya “Kiduchu” ni kuwafikia wanufaika 135,186 wanaodaiwa jumla ya shilingi bilioni 920. Kurejeshwa kwa fedha hizi, kutawezesha uendelevu wa kuwagharimia waombaji wengi zaidi wenye uhitaji, na hatimaye kuwa na raslimaliwatu wenye ujuzi, maarifa na stadi stahili katika kujenga uchumi na maendeleo ya Taifa letu.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Dk. Bill Kiwia amewasisitiza wahitimu wenye kipato kulipa mikopo yao kwani madeni yaliyoiva yamefikia shilingi trilioni 2.78 ambapo trillioni 1.84 zimekusanywa kutoka kwa wanufaika 539,103, huku bilioni 920 kutoka kwa wahitimu 135,186 zikiwa bado hazijakusanywa.

Kwa kuhitimisha makala hii, nitoe wito kwa wanufaika wahitimu wenye kipato kuwa na uzalendo kwa kujitokeza wenyewe ili kuanza kulipa mikopo yao ili kuwezesha kujenga uendelevu wa utoaji wa mikopo kwa waombaji wenye sifa wanaojiunga na vyuo vya kati na vya elimu ya juu. 

Upo umuhimu kwa wanufaika wa mikopo ya elimu waliokwishahitimu, kufahamu kuwa wanapaswa kuaza kurejesha mikopo hiyo pindi wanapopata kipato hata kama wamejiajiri wenyewe.

Dhamira njema ya serikali ya kusomesha wananchi wake itazidi kutimia endapo wanufaika watalipa kiduchu walichonacho kwa moyo wa upendo na uzalendo ili Taifa letu lizidi kusonga mbele zaidi kimaendeleo. Tafakari.

Maoni : 0620 800 462.





 

0/Post a Comment/Comments