KANISA LA MORAVIAN LATOA WITO WA AMANI NA UVUMILIVU KWA WAUMINI

........

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Kanisa la Moravian Tanzania limewataka waumini wake kutokata tamaa wala kukimbia majaribu wanapokumbana na changamoto mbalimbali, bali waendelee kumuamini Mungu huku wakidumisha amani mioyoni mwao.

Wito huo umetolewa leo Aprili 12, 2026 jijini Dodoma na Mwinjilisti wa Kanisa la Moravian Ushirika wa Kisasa, Anosisye Mwaigom, wakati wa ibada maalum ya kusifu na kuabudu iliyofuatwa na tamasha lililoshirikisha vikundi mbalimbali vya uimbaji wa nyimbo za injili.

Akihubiri katika ibada hiyo, Mwaigom alisema kuwa kuwa mshiriki wa dhehebu fulani siyo kigezo cha mtu kwenda mbinguni, bali kinachotakiwa ni kuwa na uhusiano wa kweli na Mungu. 

Alisisitiza umuhimu wa kumjua na kumtambulisha Mungu hata katikati ya changamoto, akibainisha kuwa waumini wengi hukimbia majukumu au familia zao kutokana na kutokumjua Mungu ipasavyo.

“Jaribu ni sehemu ya kukuimarisha. Ukimjua Mungu kwa dhati, hautokimbia hovyo hovyo bali utasimama imara katika imani,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mchungaji wa Ushirika wa Mkonze, Emmanuel Jonathan Mwakabalila, alisema ni muhimu kwa kanisa kuendelea kuwekeza katika huduma ya kusifu na kuabudu, akieleza kuwa huduma hiyo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha imani ya waumini na kuwalea vijana katika misingi bora ya kiroho.

Alifananisha uwekezaji huo na jitihada zinazofanywa na wazazi kuwapeleka watoto wao katika shule bora, akisema ni wakati sasa kwa waumini kuwekeza kwa nguvu sawa katika mambo ya kiroho bila kusita.

“Katika kuimba ndipo tunapoandaa vijana sahihi kwa ajili ya kulitumikia kanisa. Hii ni huduma inayohitaji kupewa kipaumbele cha pekee,” alisema Mwakabalila.

Nao baadhi ya washirika wa kanisa hilo walieleza kuwa matamasha ya kusifu na kuabudu yana mchango mkubwa katika kuijenga jamii kiroho na kijamii, huku wakiwahimiza vijana kutokata tamaa bali kuendelea kumtumaini Mungu.

Akizungumza katika tamasha hilo, muimbaji wa nyimbo za injili, Grace Kamendu, aliwataka vijana waliokata tamaa kuinuka tena na kuanza upya, akisisitiza kuwa kwa Mungu hakuna lisilowezekana.

“Linaloonekana gumu kwako si gumu kwa Mungu. Ukimtegemea, unaweza kurejeshwa na kuwa mtu mpya kabisa,” alisema.

Naye muimbaji na muinjilisti, Adam Kisimile, alisema kuwa huduma ya kusifu na kuabudu ina manufaa makubwa kwa Mkristo, ikiwemo kumuinua kiroho na kumtambulisha katika vipawa vyake.

Alieleza kuwa kupitia ibada hiyo, waumini walishuhudia matukio ya kiroho ikiwemo watu kufunguliwa na Roho Mtakatifu kufanya kazi katikati yao, jambo lililoleta faraja na kuimarisha imani kwa wengi waliohudhuria.

“Tumeona namna Mungu anavyotumia watumishi wake kufungua watu kiroho. Haya ni matunda ya kusifu na kuabudu kwa dhati,” aliongeza.

Tamasha hilo lililoambatana na nyimbo za furaha, ibada na maombi, limeelezwa kuwa chanzo muhimu cha kuimarisha mshikamano wa waumini pamoja na kukuza imani katika jamii.










 

0/Post a Comment/Comments