LONGIDO NA NGORONGORO BEGA KWA BEGA KATIKA UHIFADHI NA UTALII

.............

Na Sixmund Begashe, Dodoma 

Uongozi kutoka katika maeneo ya jamii za kifugaji Longido na Ngorongoro umekutana na uingozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii,  Jijini Dodoma kwa lengo la kupata uelewa wa pamoja kuhusu uhifadhi endelevu wa Wanyamapori pamoja na Maliasili ili kuendeleza utalii. 

Akizungumza na ujumbe huo Jijini Dodoma Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema uhifadhi na utunzaji wa Maliasili unachechemua sekta ya Utalii nchini na kuliingizia Taifa fedha za kigeni zinazowezesha kutekeleza Miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara, afya na elimu kwa faida ya Watanzania wote.

Dkt. Kijaji amesema kuwa lengo la Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha uhifadhi wa Maliasili unaenda sambamba na maendeleo ya kiuchumi ya Watanzania hivyo Wizara anayoiongoza itaendelea kushirikiana kikamilifu na viongozi hao pamoja na wananchi katika kuhakikisha Uhifadhi na Utalii unaendelea kuwanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla. 

Pamoja na kuwapongeza kwa ushirikiano wanaoutoa katika Uhifadhi, amewataka kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais Mhe. Dkt. Samia katika kulinda Maliasili zilizopo na kuziendeleza kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido Mhe. Thomas Ngobei amesema kuwa uongozi wa Halmashauri hiyo unatambu mchango wa Wizara na kwamba itaendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali hususani katika mchakato wa uwanzishwaji wa Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii Ziwa  Natron (JUHIZINA). 

Kikao hicho kimeudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi, baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wizara pamoja na wataalam wa taasisi za Wizara hiyo.

Katika hatua nyingine Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na kuutaka uongozi huo kuongeza kasi katika utekelezaji wa majukumu yake ili kufikia matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya uhifadhi, Maliasili na Utalii.










 

0/Post a Comment/Comments