......
Na Carlos Claudio, Dodoma
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imetoa tahadhari kali kwa umma kufuatia kubainika kwa matukio ya utapeli yanayofanywa na watu wanaojifanya watumishi wa wakala huo, hususan katika Mkoa wa Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na TANROADS, matapeli hao wamekuwa wakiwasiliana na wamiliki wa mabango ya matangazo (billboards) kwa njia ya simu, wakijitambulisha kama maafisa wa wakala huo na kudai fedha kwa madai ya kuzuia kuondolewa kwa mabango yaliyovuka muda wa vibali.
Imeelezwa kuwa baadhi ya wananchi tayari wameathirika kwa kutuma fedha kwa watu hao kutokana na udanganyifu huo.
TANROADS imesisitiza kuwa haitoi huduma wala kupokea malipo kupitia namba binafsi za simu au mtu mmoja mmoja, bali malipo yote hufanyika kupitia mifumo rasmi ya Serikali inayotambulika.
“Tunawaonya wananchi kuwa makini na kutotuma fedha kwa mtu yeyote anayewasiliana nao kwa njia hiyo na kujitambulisha kama mtumishi wa TANROADS bila kufuata taratibu rasmi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, wakala huo umebainisha kuwa unaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi Tanzania kuwafuatilia wahusika wa vitendo hivyo ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Wananchi wametakiwa kutoa taarifa za matukio ya aina hii kupitia ofisi za TANROADS zilizo karibu au kutumia njia rasmi za mawasiliano za wakala huo.
TANROADS imeeleza kuwa itaendelea kuchukua hatua madhubuti kulinda maslahi ya wananchi na kuhakikisha huduma zake zinatolewa kwa uwazi, usalama na uadilifu.



Post a Comment