MKUTANO WA KIKANDA WAJADILI USALAMA NA BIASHARA HARAMU YA SILAHA

 

******

Na Mwandishi Wetu,DAR ES SALAAM 

Makamu Mwenyekiti wa RECSA na ‎Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Paschal Katambi Patrobass (Mb), ameshiriki Mkutano kwa njia ya Mtandao wa Kamati Ndogo ya Mawaziri ya Kikanda, unaoshughulikia Udhibiti wa Silaha ndogo na nyepesi katika Ukanda wa Maziwa Makuu na Pembe ya Afrika (RESCA).
‎Kikao hicho, kimewakutanisha Mawaziri wa Usalama kutoka nchi wanachama, kikiwa na lengo la kujadili Hali ya Usalama katika ukanda huo pamoja na changamoto zinazoendelea kujitokeza, hususani Usambazaji na Matumizi Haramu ya Silaha ndogo na nyepesi. 

Ametoa kauli hiyo baada ya Kikao cha Saba cha nchi wanachama wa Kituo cha Kikanda Kinachoshughulika na Udhibiti wa Silaha katika Nchi za Maziwa Makuu na Pembe ya Afrika (RECSA),ngazi ya mawaziri kinachojumuisha nchi ya Tanzania,Burundi,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC), Rwanda,Uganda,Kenya,Somalia,Sudan,Sudan Kusini, Ethiopia, Eritrea, Djibouti, Jamhuri ya Kongo na Jamhuri ya Kati, kilichofanyika kwa njia ya mtandao ambapo masuala mbalimbali yalijadiliwa ikiwemo udhibiti wa silaha na kupambana na biashara haramu ya silaha.

Amesema sambamba na hilo, Serikali kupitia Wizara ya mambo ya ndani ya Nchi imejipanga kimkakati kuimarisha ulinzi na usalama wa Mifumo ya Uthibiti katika Uingizaji Silaha,Kuangalia Dhana nzima ya Umiliki na Wajibu wa Mmiliki, Tathmini ya Matumizi sahihi ya Silaha,Ukaguliwaji wa Silaha,Lengo na Dhamira ya Muombaji na Mmiliki wa Silaha, Tabia na mienendo hatarishi ya mmiliki wa Silaha na kuimarisha mifumo ya kiteknolojia na Kidigitali katika kudhibiti Silaha.

*“Nchi yetu ni nchi ya Muungano Kikatiba, yenye misingi ya kisheria, sera madhubuti, zinazochochea Amani, Mshikamano na Utulivu. Tanzania ni Nchi mwanachama wa RECSA, tumeendelea kuwahakikishia wanachama wenzetu kuwa nguzo ya amani na utulivu ndani na nje ya mipaka yetu. Tunashirikiana pamoja katika doria ili kudhibiti na kupunguza silaha ndogondogo na nyepesi zinazozunguka kinyume na sheria. Katika dhana nzima ya udhibiti wa silaha, serikali tumedhamiria kuimarisha mifumo ya uingizaji wa silaha,utambuzi wa mifumo ya uingizaji,umiliki na wajibu wa mmiliki,ukaguliwaji wa silaha,pamoja na tathmini ya matumizi sahihi ya silaha kuondoa matishio ya amani ndani na nje ya kanda ya pembe ya Afrika.” Amesema Mheshimiwa Katambi*

Mhe. Katambi pia amewataka wamiliki wa silaha hapa nchini, kuzingatia kikamilifu masharti ya umiliki wa silaha zao pamoja na kulipia leseni za silaha wanazomiliki ikiwa ni takwa la kisheria ambapo kwa mujibu wa kifungu cha 20 cha Kanuni za Udhibiti wa Silaha na Risasi za mwaka 2016 linalomtaka kila mmiliki wa silaha nchini kulipia Leseni za Bastola, Shotgun na Rifle na ada hiyo ya Leseni hulipwa kuanzia tarehe 1 Julai hadi 30 Septemba kila mwaka. 

*Ametoa agizo kwa wale wanaomiliki au kukaa na Silaha kinyume cha Sheria iwe kwa kupewa, kuokota, kurithishwa, kupora au kwa namna yoyote isivyo* *kisheria kuzisalimisha haraka katika Kituo cha Polisi au kutoa taarifa za siri kufichua umiliki wa kinyemera kwa ajili ya Usalama wa Raia na Mali zao pia Amani ya Nchi yetu.*





0/Post a Comment/Comments