Na Mwajabu Mhando
Wanawake wengi nchini Tanzania wamekuwa wakijishughulisha na biashara ndogo ndogo ili kujipatia kipato cha kujikimu na kuendesha familia zao. Miongoni mwa biashara hizo ni uuzaji wa mboga mboga na matunda katika masoko na mitaa mbalimbali wanayoishi. Biashara hii imekuwa chanzo muhimu cha kipato kwa wanawake wengi, licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Katika kufanya makala hii, nilifanya mahojiano na mwanamke muuza mboga mboga mkazi wa Tandale jijini Dar es Salaam, anayeitwa Ester George, mama wa watoto watatu. Ester anaendesha biashara yake ndogo ya kuuza mboga na matunda ili kusaidia mahitaji ya familia yake. Anasema kuwa alianza biashara hiyo miaka kadhaa iliyopita baada ya kuona kipato cha familia hakitoshi kukidhi mahitaji ya kila siku.
Katika mahojiano hayo, Ester anaeleza kuwa biashara ya mboga mboga na matunda imekuwa msaada mkubwa katika familia yake. “Kupitia biashara hii naweza kununua chakula nyumbani, kusaidia ada za watoto na gharama nyingine za familia. Mume wangu hana kazi yenye kipato kikubwa, hivyo biashara yangu imekuwa msaada mkubwa kwa familia yetu,” anasema Ester.
Licha ya mchango huo, wanawake wengi wanaofanya biashara ya mboga na matunda hukumbana na changamoto mbalimbali. Miongoni mwa changamoto hizo ni mtaji mdogo, ushindani mkubwa katika masoko, pamoja na uharibifu wa bidhaa hasa matunda na mboga zinazoharibika haraka. Pia wateja wengine huchukua bidhaa kwa mkopo lakini hushindwa kulipa kwa wakati, jambo linalopunguza mtaji wa wafanyabiashara hawa.
Mbali na changamoto hizo za kiuchumi, wanawake hawa pia hukumbana na changamoto za unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo yao ya kazi. Baadhi yao hukumbana na maneno ya kudhalilisha, vitisho au hata vishawishi visivyofaa kutoka kwa baadhi ya wanaume wanaowazunguka katika maeneo ya biashara.
Ester anaeleza kuwa hali hiyo wakati mwingine huwafanya wanawake kufanya kazi katika mazingira yasiyo salama. Kwani yeye amekuwa ni mmoja kati ya wahanga waliokumbana na changamoto hizo ikiwemo kuitwa majina yasiyofaa na wakati mwingine baadhi ya watu kumdhania kwamba yeye si mwanamke anayependa kutulia nyumbani kwake.
Kwa upande wa serikali, juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika kusaidia wanawake wafanyabiashara wadogo. Afisa wa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii katika halmashauri anasema wao hutoa elimu kuhusu haki za wanawake, mbinu za kujilinda dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, pamoja na kuwahamasisha wanawake kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ili waweze kupata mikopo ya riba nafuu. Pia serikali imekuwa ikitoa mafunzo ya ujasiriamali ili kuwasaidia wanawake hawa kuboresha biashara zao.
Wadau wengine ambao wamekuwa wakitetea haki na usawa wa wanawake nchini ikiwemo Chama cha Wanawake Wanahabari Tanzania (TAMWA), kupitia Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo Dr. Rose Reuben katika kilele hicho cha siku ya wanawake amesema licha ya uwepo wa changamoto nyingi kwa wanawake wauzaji wa mboga mboga ikiwemo upungufu wa usalama , kukosekana kwa soko la uhakika na hata upatikanaji hafifu wa bidhaa lakini bado wanaendelea kuwapa elimu wakishirikiana na benki ya CRDB kwani wanawake wengi wajasiriamali wameahidi kupokea elimu hiyo na kuendelea kuitumia huku kipaumbele cha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kikizingatiwa ili kufikia usawa katika Nyanja zote za kijamii.
Aidha, taasisi mbalimbali za kifedha ikiwemo Benki ya CRDB imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha wanawake wajasiriamali kupitia huduma za kifedha jumuishi, mikopo nafuu, pamoja na mafunzo ya ujasiriamali ikiwemo kupitia programu zake mbalimbali.
CRDB katika siku maalumu ya wanawake duniani ambayo waliungana na wanawake wajasiriamali kwa kushirikiana na TAMWA kupitia Meneja usimamizi wa mafunzo ambaye ni Joshua Mwakalobo amesema wataendelea kutoa elimu ya fedha na ujasiriamali ili kuwainua vijana na wanake wajasiriamali pamoja na kuwawezesha kifedha ili kuijua thamani ya pesa na mafanikio.
Kwaujumla benki hiyo imefanikiwa kuwainua wanawake hawa kwa kuwapatia
mitaji na ujuzi unaowawezesha kukuza biashara zao, kuongeza kipato, na
kuboresha maisha yao na jamii inayowazunguka kwa ujumla.
Wanawake wanaouza mboga mboga na matunda pia wana mchango mkubwa katika jamii na uchumi. Wanachangia upatikanaji wa chakula kwa urahisi katika maeneo ya mijini na vijijini, wanazalisha ajira binafsi, na kusaidia familia zao kupata mahitaji muhimu kama chakula, elimu na huduma za afya. Biashara hizi ndogo ndogo pia huchangia mzunguko wa fedha katika jamii.
Katika mafanikio hayo, mchango wa wanaume nao ni muhimu. Wanaume wanaweza kuwasaidia wake zao kwa kuwapa ushirikiano, kuwaheshimu katika kazi zao, pamoja na kuwasaidia katika majukumu ya familia ili wanawake waweze kuendesha biashara zao kwa utulivu. Ushirikiano wa wanandoa katika shughuli za kiuchumi unaweza kuimarisha ustawi wa familia kwa ujumla.
Kutokana na hali hiyo, jamii inapaswa kuthamini na kuheshimu kazi zinazofanywa na wanawake hawa, huku ikiendelea kupinga vitendo vyote vya unyanyasaji wa kijinsia. Wanawake nao wanahimizwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kujiunga katika vikundi vya maendeleo na kutumia fursa za mafunzo na mikopo zinazotolewa na serikali na taasisi mbalimbali.
Kwani takwimu mbalimbali za kiuchumi ikiwemo Global Enterpreneurship kwa mwaka 2024 inaonesha kuna ongezeko la wanawake katika umiliki wa biashara ndogo ndogo ambazo zimekua ni sehemu mojawapo inayochangia kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja, familia na hata Taifa kwa ujumla.
Kwa ujumla,
wanawake wauzaji wa mboga mboga na matunda ni sehemu muhimu ya maendeleo ya
familia na jamii. Kwa kupewa mazingira salama ya kufanya biashara pamoja na
msaada kutoka kwa jamii na serikali, wanaweza kuendelea kuchangia kwa kiwango
kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi, wakati nchi ikikua ni vyema
kuhakikisha usalama wa wanawake na jamii nzima kwa ujumla. Kwa pamoja TUMLINDE
MWANAMKE ILI TUILINDE JAMII YETU SOTE.
Post a Comment