PANDA BEI YA MAFUTA: CCM YATOA MAPENDEKEZO MAZITO KULINDA WANANCHI

........

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeitaka serikali kuchukua hatua za haraka na madhubuti kulinda uchumi wa wananchi kufuatia kupanda kwa bei za mafuta nchini na duniani kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 7, 2026 jijini Dodoma, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Kihongosi, amesema chama hicho kinapendekeza kutengwa kwa ruzuku ya mafuta pamoja na kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa nishati utakaosaidia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya bei pindi zinapotokea.

Amesema mfuko huo utakuwa na lengo la kupunguza makali ya ongezeko la bei za mafuta katika soko la dunia na kusaidia kudhibiti athari zake kwa wananchi na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Aidha, CCM imeitaka serikali kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala na kupunguza utegemezi wa mafuta katika ofisi za serikali na sekta binafsi, ili kuongeza uwezo wa kujitegemea wakati wa changamoto za nishati.

Katika hatua nyingine, Kihongosi amesisitiza umuhimu wa kuwa na akiba ya kimkakati ya mafuta ili kuhakikisha upatikanaji wake unakuwa wa uhakika wakati wote, hata panapotokea misukosuko ya soko la kimataifa.

Pia ameitaka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kusimamia kikamilifu sekta ya mafuta ili kuzuia uchepushaji, kuongeza uwazi, na kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unakuwa wa uhakika na ufanisi.

Vilevile, amehimiza kuimarishwa kwa uwekezaji katika miundombinu ya kuhifadhi mafuta pamoja na kuongeza vituo vya mafuta kwa kushirikiana na sekta binafsi, hatua itakayosaidia kuimarisha usambazaji wake nchini.

Kuhusu sera za nishati, Kihongosi amesema serikali inapaswa kuangalia uwezekano wa kutoa ruzuku ya mafuta huku ikiendelea kuhimiza matumizi ya nishati mbadala, hususan gesi asilia, ili kupunguza utegemezi wa mafuta kutoka nje ya nchi.

Pia amependekeza kuanzishwa kwa mfuko wa kuendeleza utafutaji na uchimbaji wa mafuta nchini ili kuhakikisha taifa linakuwa na uhakika wa nishati kwa muda mrefu.

Akihitimisha, Kihongosi amewataka Watanzania kutambua kuwa kupanda kwa bei za mafuta ni changamoto ya kimataifa na si suala la kisiasa, akisisitiza kuwa licha ya wito wa kupunguza baadhi ya tozo, ushuru una jukumu muhimu katika kugharamia maendeleo ya taifa.



 

0/Post a Comment/Comments