Na Carlos Claudio, Dodoma.
Wanawake nchini wamehimizwa kujitokeza kwa wingi na kuwa mfano wa mwanamke wa imani, hekima na ujasiri kama Abigaeli wa Biblia, ili kusaidia kuleta mabadiliko chanya katika familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Mchungaji wa Calvary Assemblies of God, Mch. Felichismus Tarimo, alipokuwa akifungua kongamano la kwanza la wanawake lenye kaulimbiu ya “Wito Maalum kwa Wanawake: Utumishi wa Pamoja kwa Umoja, Mshikamano, Upendo na Amani” linaloandaliwa na huduma ya Global Women Ministry Africa (GLOWMA).
Akizungumza katika kongamano hilo, Mch. Tarimo alisema ipo haja kwa wanawake wa Tanzania kuwa na moyo wa haraka wa kumkimbilia Mungu wanapoona changamoto katika jamii, wakifuata mfano wa Abigaeli ambaye alichukua hatua ya haraka kuzuia madhara makubwa.
Alieleza kuwa wanawake wa aina hiyo wana nafasi kubwa ya kusaidia kupunguza hasira ya Mungu juu ya taifa kwa njia ya maombi, toba na kusimama katika haki.
“Bwana anainua kizazi cha wanawake wenye hekima na utayari wa kuchukua hatua. Wanawake watakaoona hali ya mambo yanavyoenda na kufanya haraka kumkimbilia Mungu, wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika taifa,” alisema.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa wanawake kujifunza na kuelewa Neno la Mungu ili waweze kusimama imara kiroho na kuwa msaada sahihi katika familia na jamii.
Kwa upande wake, Mwanzilishi na Rais wa GLOWMA, Mtume Prof. Margareth Kilimali, alisema mwanamke asiye na maarifa ya Neno la Mungu hawezi kutimiza wajibu wake ipasavyo katika familia na jamii.
Alinukuu maandiko akieleza kuwa maarifa ya kweli yanatokana na Neno la Mungu, na kusisitiza kuwa kukosekana kwa maarifa hayo kunaweza kuathiri hata vizazi vijavyo.
“Ni muhimu mwanamke akajijenga katika maarifa ya Neno la Mungu ili aweze kumshauri mtoto, mume na jamii kwa ujumla. Bila maarifa hayo, ni vigumu kutekeleza kusudi la Mungu katika maisha yake,” alisema.
Katika mada yake kuhusu kuinua viwango vya waombaji, Prof. Kilimali alieleza kuwa kongamano hilo linalenga kuwawezesha wanawake kiroho, kuwaunganisha na kuwajengea uwezo wa kuwa viongozi bora katika jamii na Kanisa.
Alitoa shukrani kwa viongozi wa Dodoma na washiriki wote kwa kujitoa kwao kuhakikisha mafanikio ya kongamano hilo, akisisitiza kuwa umoja na mshikamano ni msingi muhimu katika kufanikisha kazi za Mungu.
Akifafanua zaidi, alisema GLOWMA ni huduma ya wanawake barani Afrika inayolenga kuwaunganisha wanawake watumishi wa Mungu ili washirikiane kuifikia jamii kwa Neno la Mungu na matendo ya huruma.
Huduma hiyo ilianzishwa mwaka 2005 nchini Kenya na baadaye kusambaa katika nchi mbalimbali za Afrika, ikiwemo Tanzania ambako ilipata usajili rasmi mwaka 2012.
Maono ya huduma hiyo ni kuwawezesha wanawake kuwa nuru ya ulimwengu, kukuza umoja na upendo, pamoja na kutoa mafunzo ya uongozi na huduma kwa makundi mbalimbali ya kijamii.
Kongamano hilo linaendelea kufanyika katika eneo la Chamwino, mkoani Dodoma, na linatarajiwa kufikia kilele chake Jumamosi, likiwahamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki na kunufaika na mafundisho mbalimbali ya kiroho.




Post a Comment