*****
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema mafanikio makubwa yanayoonekana katika sekta ya mawasiliano na TEHAMA yametokana na uwezeshaji na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuweka mazingira wezeshi yanayovutia uwekezaji na kuongeza upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo bungeni jijini Dodoma Aprili 30, 2026, Waziri Kairuki amssema uwekezaji huo umechochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa kidijitali na kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini.
"Nnamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuona umuhimu wa Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kuweka mazingira wezeshi yanayovutia uwekezaji ambayo yamewezesha upatikanaji wa fedha katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kisekta ambayo utekelezaji wake unachochea ukuaji wa Uchumi wa Kidijitali" alisema Waziri Kairuki
Akifafanua zaidi Waziri Kairuki amesema, katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, sekta ya mawasiliano imepiga hatua kubwa ikiwemo kukamilika kwa ujenzi wa minara 758 katika kata 688, hatua inayowanufaisha wananchi takribani milioni 8.5.
Aidha, minara 304 iliyokuwa ya teknolojia ya 2G imeongezewa uwezo na kufikishwa 2G/3G/4G, na hivyo kuwafikia wananchi milioni 4.2 ndani ya kipindi chake cha uongozi.
Waziri Kairuki ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mradi wa Mawasiliano Vijijini unaohusisha ujenzi wa minara 636 katika kata 443. Hadi sasa, minara 456 sawa na asilimia 72 imekamilika, ambapo minara 342 tayari imewashwa na inatoa huduma kwa wananchi.
Minara 114 iliyosalia inatarajiwa kuwashwa ifikapo Juni 2026 baada ya ufungaji wa vifaa kukamilika.
Aidha, minara 180 iliyobaki inatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2026, hatua ambayo itawawezesha wananchi takribani milioni 2.5 kufikiwa na huduma za mawasiliano.
Waziri Kairuki amesema mafanikio haya ni uthibitisho wa dhamira ya Rais Samia katika kuijenga Tanzania ya kidijitali, yenye miundombinu imara na huduma za mawasiliano zinazowafikia Watanzania wote.




Post a Comment