Na Carlos Claudio, Dodoma.
Serikali imewataka wadau wa sekta binafsi ya afya nchini kuongeza ubora wa huduma, kuwekeza katika elimu ya afya kwa jamii, na kuzingatia maadili ya taaluma ili kusaidia kufikia lengo la huduma bora za afya kwa wote.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Florence Samizi, alipokuwa akimwakilisha Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, katika Mkutano wa Wadau wa Sekta Binafsi ya Afya.
Dkt. Samizi amesema sekta binafsi ina nafasi kubwa ya kuwafikia wananchi na kuchangia mabadiliko chanya katika afya ya Watanzania, akibainisha kuwa pamoja na juhudi za serikali katika kuboresha miundombinu na vifaa tiba, bado kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza katika kinga.
“Ni kweli tumenunua na tutaendelea kununua vifaa vya kisasa, lakini hatuwezi kufanya hivyo milele. Maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhimiza mabadiliko ya tabia ili kuzuia magonjwa yasiyoambukiza,” amesema.
Ameongeza kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka kutokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha, hali inayoongeza gharama za matibabu, huku akisisitiza kuwa yanaweza kuzuilika kupitia kinga na elimu sahihi kwa jamii.
Katika kuimarisha uelewa huo, Dkt. Samizi amewataka wamiliki wa vituo binafsi kuanzisha vitengo maalum vya elimu ya afya kwa jamii ili kusaidia wananchi kujua namna ya kujikinga na magonjwa pamoja na kufuatilia viashiria muhimu vya afya zao mapema.
Aidha, amesema serikali inaandaa programu maalum zitakazowezesha wananchi kuelewa vipimo vya msingi vya afya zao, hatua itakayosaidia kuchukua tahadhari mapema kabla ya hali kuwa mbaya.
Akizungumzia uendeshaji wa vituo vya afya, amesisitiza kuwa huduma za afya si biashara ya kawaida, bali zinahitaji kuendeshwa kwa kuzingatia sheria, usajili sahihi na viwango vinavyotakiwa ili kulinda usalama wa wagonjwa.
Pia ameahidi kuwa serikali inaendelea kupitia mfumo wa tozo na ada mbalimbali ili kuhakikisha unakuwa rafiki zaidi kwa wawekezaji wa sekta binafsi bila kuathiri ubora wa huduma.
Kuhusu maendeleo ya sekta hiyo, Dkt. Samizi amegusia kuibuka kwa huduma mpya kama vituo vya mazoezi (fitness centers), akisema serikali inaweka mikakati ya kuhakikisha vinazingatia viwango na usalama wa watumiaji.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ni muhimu katika kufanikisha malengo ya afya kwa wote, akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya huduma za afya nchini zinachangiwa na sekta binafsi, jambo linaloifanya kuwa mshirika muhimu wa serikali.
“Hatuna budi kushirikiana, hakuna nchi inayoweza kufanikiwa bila ushirikiano. Serikali pekee haiwezi,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Gakala Health Centre, Gunda Gakala, ameishukuru serikali kwa ushirikiano wake, akisema kituo hicho kinaendelea kutoa huduma mbalimbali ikiwemo za wagonjwa wa nje (OPD), wagonjwa wa ndani (IPD), pamoja na huduma za meno, macho na upasuaji.
Amesema ushiriki wao katika mkutano huo umewawezesha kubadilishana uzoefu na wadau wengine, kujifunza mbinu bora za utoaji huduma, pamoja na kupata maarifa mapya kutoka kwa wataalamu waliobobea kimataifa.
Naye Dkt. Saidi Ally Saidi kutoka kampuni ya Afya Plus, Dar es Salaam, amesema mjadala wa mkutano huo umeangazia pia matumizi ya teknolojia ya kidijitali ikiwemo akili bandia (AI) katika kuboresha huduma za afya.
Ameeleza kuwa teknolojia hiyo ina nafasi kubwa katika kufanikisha sera ya huduma za afya kwa wote, kwa kusaidia kuongeza ufanisi, usahihi wa uchunguzi na upatikanaji wa huduma kwa wananchi wengi zaidi.
Mkutano huo umefanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Kuimarisha ubora na weledi katika utoaji wa huduma za afya binafsi kuelekea kufikiwa kwa huduma za afya kwa wote nchini Tanzania.”
Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mkazo katika kuboresha sekta ya afya, huku ikihimiza ushiriki mpana wa sekta binafsi kama nguzo muhimu ya maendeleo ya huduma za afya nchini.







Post a Comment