Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imeipa Tume ya Ushindani (FCC) jukumu la kusimamia kikamilifu mikataba ya walaji ili kuondoa masharti kandamizi. Lengo ni kuhakikisha haki za walaji zinalindwa katika kila hatua ya ununuzi wa bidhaa na huduma.
Hatua hiyo inalenga kudhibiti mikataba isiyo na usawa inayowaumiza walaji. Serikali imeonya kuwa haitavumilia vitendo vya upande mmoja kujinufaisha kupitia mikataba hiyo.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga (Mb.), alitoa maagizo hayo Aprili 2, 2026 jijini Dar es Salaam. Tukio hilo lilifanyika katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Haki za Mlaji Duniani.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga
Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameielekeza FCC kukamilisha utafiti wa biashara mtandao nchini. Matokeo ya utafiti huo yatasaidia kuunda mkakati madhubuti wa sekta hiyo.
Alisema mkakati huo utaongeza uwazi kwenye biashara za kidijitali. Pia utavutia uwekezaji na kuimarisha usalama wa walaji.
Waziri Kapinga pia amesisitiza ushirikiano kati ya FCC na taasisi nyingine za udhibiti. Zikiwemo TBS na WMA katika kukabiliana na ukiukwaji wa haki za walaji.
Alisema elimu kwa umma ni nyenzo muhimu katika mapambano hayo. Hivyo, taasisi hizo zinapaswa kuongeza juhudi za kutoa uelewa kwa wananchi.
Katika kuendana na teknolojia, Waziri huyo alipongeza uzinduzi wa ‘FCC Kiganjani’. Jukwaa hilo la WhatsApp linalenga kurahisisha mawasiliano kati ya walaji na tume.
Aidha, FCC imetakiwa kuimarisha matumizi ya mitandao ya kijamii kutoa elimu. Pia kuanzisha klabu mashuleni ili kuwajengea vijana uelewa mapema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa FCC, Dkt. Aggrey Mlimuka, alisema tume iko tayari kutekeleza maagizo hayo. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na wadau mbalimbali.
Kaimu Mkurugenzi wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, alisema elimu kwa walaji inaendelea kutolewa. Alisema hatua hiyo inawawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi wanaponunua bidhaa na huduma.



















Post a Comment