SERIKALI YATANGAZA TUZO KUBWA YA WAANDISHI – MILIONI 10 KUSHINDANIWA

........

Na Carlos Claudio, Dodoma

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza rasmi kuanza kwa hatua ya mwisho ya utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Julius Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2026, huku hafla ya utoaji wa tuzo hizo ikitarajiwa kufanyika Aprili 13, 2026 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 8, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda amesema tuzo hiyo hutolewa kila mwaka ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, ambaye pia alitambulika kama nguli wa uandishi bunifu na mdau mkubwa wa kukuza lugha ya Kiswahili.

Amesema kuwa hafla hiyo ya nne ya utoaji wa tuzo hizo itafanyika katika Ukumbi wa The Super Dome uliopo Masaki, jijini Dar es Salaam, ambapo mwaka huu washindani wamechuana katika nyanja nne ambazo ni ushairi, riwaya, hadithi za watoto na tamthilia.

Profesa Mkenda ameeleza kuwa maandalizi ya tuzo hiyo yameratibiwa kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania kwa kushirikiana na Kamati Kuu ya Tuzo, inayongozwa na Penina Mlama, huku akibainisha kuwa mwaka huu mgeni rasmi anatarajiwa kuwa msanii na mshairi maarufu kimataifa, Abdulatif Abdalla, ambaye ana uzoefu mkubwa katika fasihi na aliwahi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 15.

Kwa upande wake, Profesa Mlama amesema mchakato wa tuzo hiyo umehusisha upokeaji na uchambuzi wa miswada kwa kipindi cha mwaka mzima, ukifanywa na jopo la majaji waliobobea katika taaluma ya fasihi. Amesema orodha teule ya washindani tayari imekamilika na washindi watatu kwa kila kipengele watatangazwa rasmi siku ya hafla.

Ameongeza kuwa mwitikio wa washiriki mwaka huu umekuwa mkubwa, ukiwashirikisha Watanzania kutoka maeneo mbalimbali ya nchi pamoja na washiriki kutoka nje ya nchi, ikiwemo Jamhuri ya Czech, jambo linaloonyesha kukua kwa ushawishi wa tuzo hiyo kimataifa.

Kuhusu zawadi, amesema mshindi wa kwanza katika kila kipengele atapata shilingi milioni 10, pamoja na kuchapishiwa muswada wake na serikali kununua nakala kwa ajili ya shule na maktaba za taifa, huku pia akipatiwa ngao na cheti. Mshindi wa pili atazawadiwa shilingi milioni 7 na cheti, na mshindi wa tatu atapata shilingi milioni 5 pamoja na cheti.

Akimhitimisha, Profesa Mlama ametoa wito kwa wananchi na wadau wa fasihi kuendelea kuunga mkono na kuitangaza tuzo hiyo ili kuongeza ushiriki wa Watanzania katika kukuza na kuendeleza uandishi bunifu nchini.



 

0/Post a Comment/Comments