*******
Na Mwandishi wetu
Shirika la Posta Tanzania na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wame saini makubaliano ya ushirikiano, lengo ikiwa ni kuboresha na kurahisisha huduma za maombi ya mikopo kwa wanafunzi nchini.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Mbodo, alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya majadiliano ya kina kati ya taasisi hizo mbili, yakilenga kuhakikisha vijana wanapata huduma kwa urahisi zaidi.
Bw. Mbodo alisema kupitia ushirikiano huo, ofisi za posta kote nchini zitatumika kuwasaidia waombaji wa mikopo kujaza na kuwasilisha fomu pamoja na nyaraka zinazohitajika, hatua itakayosaidia kupunguza changamoto zilizokuwa zikiwakumba baadhi ya vijana katika mchakato wa maombi.
“Baada ya majadiliano ya kina kati ya sisi Posta na Bodi ya Mikopo, hivi punde mtashuhudia tukisaini makubaliano yatakayoboresha huduma za maombi ya mikopo kwa vijana wetu. Hakuna sababu yoyote kwa waombaji kushindwa kujaza fomu au kukosa mikopo kutokana na changamoto za kiufundi,” alisema Bw. Mbodo.
Alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita imejipanga kuhakikisha vijana wanapata fursa za elimu ya juu, huku Shirika la Posta likiwa tayari kutoa mwongozo sahihi kwa waombaji ili kuhakikisha wanatimiza vigezo vyote vinavyotakiwa.
Aidha, alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB kwa mageuzi makubwa yanayoendelea kufanywa katika taasisi hiyo, akibainisha kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Bw. Mbodo aliongeza kuwa miundombinu ya posta ipo tayari na imeboreshwa kwa huduma za kisasa, ikiwemo mfumo wa kidijitali unaowezesha wananchi kupata huduma popote walipo, hali itakayorahisisha utekelezaji wa jukumu hilo jipya.
Alisema wataalamu wa posta katika ngazi zote kuanzia wilaya hadi mikoa wameandaliwa kikamilifu kutoa huduma hiyo kwa ufanisi, kuhakikisha hakuna kijana anayekosa mkopo kutokana na kushindwa kukidhi taratibu za maombi.
Kwa upande mwingine, Bw. Mbodo alisisitiza kuwa ushirikiano huo unaonesha dhamira ya taasisi za umma kufanya kazi kwa pamoja katika kuhudumia wananchi, akieleza kuwa serikali ni moja na taasisi zake zina jukumu la pamoja la kuhakikisha huduma bora zinawafikia Watanzania.
Alitumia fursa hiyo kuwaalika wadau wengine kushirikiana na Shirika la Posta Tanzania kufikisha huduma zao kwa wananchi kwa kutumia mtandao mpana wa ofisi zake uliopo nchi nzima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dkt. Bill Kiwia, alisema ushirikiano huo unaendana na mabadiliko yanayofanywa na taasisi hiyo katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wanafunzi.
Dkt. Kiwia alisema hapo awali baadhi ya waombaji walikuwa wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kutegemea huduma za mitandao katika maeneo yasiyo na uhakika, jambo lililosababisha wengine kushindwa kukamilisha maombi yao kwa wakati.
“Tumebaini vijana wetu wanapata taabu katika mchakato wa kuomba mikopo, wengine hulazimika kwenda mbali kutafuta huduma za intaneti au kutumia vifaa visivyo na uhakika. Hali hii imekuwa ikiathiri ukamilishaji wa maombi kwa wakati,” alisema Dkt. Kiwia.
Alieleza kuwa kupitia makubaliano hayo, Shirika la Posta litasaidia kutoa huduma za maombi ya mikopo kupitia ofisi zake zaidi ya 360 zilizopo nchi nzima, hali itakayorahisisha upatikanaji wa huduma hizo hata kwa waombaji walioko maeneo ya vijijini.
Aidha, alisema ushirikiano huo utawezesha pia huduma za uhakiki wa nyaraka na taarifa za waombaji kufanyika kwa urahisi zaidi, jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi na kupunguza changamoto zilizokuwepo hapo awali.
“Lengo letu ni kuhakikisha kila kijana mwenye sifa anaweza kuomba mkopo kwa wakati na kukamilisha maombi yake ipasavyo. Kupitia ushirikiano huu, tutarahisisha mchakato mzima kuanzia maombi hadi upatikanaji wa taarifa sahihi,” aliongeza.
Hata hivyo, Dkt. Kiwia alisisitiza kuwa waombaji bado wanaweza kutumia mifumo ya mtandao kuwasilisha maombi yao, lakini wale watakaohitaji msaada wanahimizwa kutembelea ofisi za posta ili kupata mwongozo wa kitaalamu.
Aliitoa wito kwa vijana kutumia fursa hiyo kikamilifu pindi dirisha la maombi litakapofunguliwa, akibainisha kuwa taasisi hizo zimejipanga kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi mkubwa.




Post a Comment