TEA, WIZARA YA ELIMU ZANZIBAR KUSHIRIKIANA KUIMARISHA MIRADI YA ELIMU

Naibu Katibu Mkuu (Taaluma) Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt. Mwanakhamis Ameir (kulia) na Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dkt. Erasmus Kipesha (kushoto) wakisaini mkataba maalum kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu visiwani Unguja na Pemba.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar zimesaini mkataba maalum wa kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya elimu itakayohusisha ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia katika shule 20 za sekondari visiwani Unguja na Pemba.

Hafla ya utiaji saini imefanyika katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mazizini, Unguja ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu (Taaluma) Dkt. Mwanakhamis Ameir na Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania Dkt. Erasmus Kipesha.

Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa mkataba huo Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Erasmus Kipesha alisema, jukumu kuu la mamlaka hiyo ni kutafuta rasilimali fedha na vifaa kutoka kwa wadau wa maendeleo ya sekta ya elimu ili kuboresha miundombinu ya elimu nchini.

Alibainisha kuwa tayari fedha zimepatikana kupitia wadau hao akiwemo UNICEF na kusisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.“Fedha tayari zipo kutoka kwa wadau wetu, hivyo ni wajibu wenu kuhakikisha miradi hii inatekelezwa ipasavyo na kukamilika kwa wakati,” alisema Dkt. Kipesha.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu (Taaluma) wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt. Mwanakhamis Ameir, aliishukuru TEA kwa kuendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya elimu visiwani humo.

Alisema licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali, bado kuna changamoto kubwa katika sekta hiyo hivyo ushirikiano huo ni muhimu katika kuzitatua.

Dkt. Ameir alisisitiza kuwa, wizara iko tayari kuanza utekelezaji wa miradi hiyo mara moja huku akiwataka wataalamu wote wanaohusika kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha miradi haikwamishwi.

“Ni muhimu kuthamini ushirikiano huu na kuhakikisha thamani ya fedha inayowekezwa inaonekana kupitia utekelezaji bora wa miradi,” aliongeza.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa awali na Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi ya Elimu Bw Masozi Nyirenda, TEA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya uboreshaji wa miundombinu ya elimu katika visiwa vya Unguja na Pemba. 

Awali, takribani shilingi bilioni 3.2 zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule za amali, huku bilioni 2.5 zikielekezwa katika ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na maabara za sayansi katika shule 20.

Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dkt. Erasmus Kipesha akisaini mkataba maalum wa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu visiwani Unguja na Pemba.
Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi ya Elimu kutoka TEA Bw Masozi Nyirenda akitoa taarifa fupi kuhusu ufadhili wa miradi ya elimu visiwani Unguja na Pemba.

Baadhi ya wataalamu kutoka TEA wakijadiliana jambo wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba maalum wa utekelezaji wa miradi ya elimu visiwani Unguja na Pemba.

Naibu Katibu Mkuu (Taaluma) Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt. Mwanakhamis Ameir (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dkt. Erasmus Kipesha (wa pili kushoto) wakibadilishana mkataba wa utekelezaji wa miradi ya elimu visiwani Unguja na Pemba mara baada ya kusainiwa. Kulia ni Mwanasheria wa Wizara Bi. Khadija Chamnda na kushoto ni Meneja huduma za Sheria TEA Bi. Christina Meela.

0/Post a Comment/Comments