TRA YAZINDUA AWAMU YA PILI YA MPANGO WA MAWAZO BUNIFU

****

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua rasmi awamu ya pili ya mpango wa kupokea mawazo bunifu kutoka kwa wananchi, ikilenga kuongeza ubunifu, uwazi na ushirikishwaji katika kuboresha mifumo ya kodi nchini. Uzinduzi huo umefanyika Aprili 29, 2026 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, aliwashukuru washiriki wapatao 5,600 walioshiriki awamu ya kwanza kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania. Amesema mchango wao umeweka msingi imara wa kuendeleza mpango huo.

Mwenda alieleza kuwa awamu ya pili imeboreshwa zaidi kwa kuhakikisha mchakato wake unakuwa huru, wazi na unaoaminika. Alisisitiza kuwa mawazo yote yatakayowasilishwa yatafanyiwa uchambuzi wa kitaalamu ili kupata yale bora zaidi kwa utekelezaji.

“Tumeboresha zaidi mfumo huu ili kuhakikisha kila hatua ya wazo inafuatiliwa na kutoa matokeo ya haki kwa washiriki,” amesema Mwenda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango wa TRA, Dkt. Ephraim Mdee, amesema mfumo mpya sasa ni wa kidijitali, hatua itakayorahisisha upokeaji na ufuatiliaji wa mawazo.

Amefafanua kuwa kupitia mfumo huo wa mtandaoni, washiriki wataweza kuona hatua zote za mchakato wa mawazo yao kuanzia kupokelewa hadi uamuzi wa mwisho.

Mdee ameongeza kuwa maboresho hayo yataongeza uwazi na kuwapa washiriki fursa ya kufahamu kwa urahisi maendeleo ya mawazo yao, iwe yamefanikiwa au hayakufuzu.

TRA imesisitiza kuwa lengo kuu la mpango huo ni kuirudisha taasisi hiyo kwa wananchi kwa kuwashirikisha moja kwa moja katika usimamizi na maboresho ya mifumo ya kodi.

Aidha, imeelezwa kuwa kodi zinazokusanywa ni mali ya wananchi na hutumika kugharamia maendeleo ya taifa, hivyo ushiriki wao ni muhimu katika kuhakikisha mifumo hiyo inakuwa bora zaidi.








0/Post a Comment/Comments