ULEGA AFUNGUKA: MAWAZO MAPYA 561 YAIBUKA KUPAMBANA NA MSOGAMANO

.......

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema Serikali imepokea jumla ya bunifu 561 kutoka kwa wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na wananchi wasiokuwa wanafunzi, zenye lengo la kutatua changamoto ya msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Ulega ameeleza kuwa bunifu hizo zimepatikana kupitia shindano maalum lililolenga kuibua mawazo mapya ya kitaalamu na kibunifu kutoka kwa vijana na jamii kwa ujumla. Lengo kuu la shindano hilo ni kusaidia kupunguza foleni ambayo imekuwa kero kubwa kwa wakazi wa jiji hilo.

Aidha, Waziri Ulega amebainisha kuwa Serikali ipo katika hatua ya kuchambua bunifu hizo ili kubaini mawazo yenye tija zaidi yatakayoweza kutekelezwa kwa haraka na kwa ufanisi. Amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kushirikisha wadau mbalimbali katika kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto ya usafiri mijini.

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega ameweka wazi kuwa Serikali imeongeza thamani ya zawadi kwa washindi watakaopatikana katika shindano hilo, ikiwa ni njia ya kuhamasisha ubunifu na ushiriki mpana zaidi wa vijana na wananchi katika kutoa suluhisho bunifu kwa maendeleo ya taifa.
 

0/Post a Comment/Comments