VITONGOJI VYOTE TANZANIA BARA KUWA NA UMEME IFIKAPO MWAKA 2030- WAZIRI NDEJEMBI

******
Serikali imedhamiria kuhakikisha vitongoji vyote 64,359 vya Tanzania Bara vinafikishiwa umeme ifikapo mwaka 2030 ili kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii vitongojini pamoja na utoaji wa huduma bora katika maeneo hayo.

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema hayo Aprili 22, 2026 Bungeni Jijini Dodoma wakati anawasilisha taarifa ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 katika Bunge la 13 Mkutano wa Tatu, Kikao cha Kumi na Nne.

“Mwelekeo wa Serikali ni kuhakikisha umeme unafikishwa katika vitongoji vyote Tanzania Bara na ili kufikia azma hiyo, Serikali ilianza utekelezaji wa mradi mkubwa wa kupeleka umeme katika Vitongoji 9,009 ambao utakamilika katika kipindi cha miaka mitatu ijayo,” amesema Waziri Ndejembi.

Amefafanua kuwa miradi inayoendelea kutekelezwa ya kupeleka umeme vitongojini itawezesha vitongoji 50,453 sawa na asilimia 78.4 ya vitongoji vyote vya Tanzania Bara kufikishiwa huduma ya umeme ifikapo mwaka 2028, hatua ambayo itachochea kasi ya ukuaji wa uchumi vitongojini.

Waziri Ndejembi ametaja hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika kupeleka nishati vijijini ni kuwa ni pamoja na kuanza utekelezaji wa mradi wa kuongeza uunganishaji wa wateja katika vitongoji (Universal Hamlet Eletrification and Last Mile Customers Connectivity) katika mikoa ya Pwani, Morogoro na Dodoma ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mahsusi wa Nishati wa Taifa (National Energy Compact) ulioridhiwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika (Mission 300) mwezi Januari, 2025.

Hatua nyingine ni utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji 3,060 sawa na vitongoji 15 kwa kila Jimbo ambao amesema umefikia 80% ya utekelezaji.

“Serikali iliendelea na utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme katika Vitongoji vya Mikoa ya Songwe, Kigoma na Lindi pamoja na maeneo ya migodi midogo ikiwemo iliyopo Chunya (Mbeya) na Kwa Msisi Handeni (Tanga) na viwanda na kilimo katika Mikoa ya Ruvuma, Njombe, Mbeya na Rukwa ili kuchochea shughuli za kiuchumi katika mikoa hiyo, ambapo utekelezaji upo hatua mbalimbali,” amebainisha Waziri Ndejembi.

Katika kuhakikisha kuwa maeneo yaliyo mbali na Gridi ya Taifa yanafikiwa na huduma za umeme Waziri Ndejembi amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) iliendelea na utekelezaji wa mradi wa kusambaza mifumo ya jua inayojitegemea (Solar Home System-SHS) katika makazi 20,000 katika visiwa vidogo 143 vilivyopo katika Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika ambapo hadi Machi, 2026 jumla ya makazi 1,302 yalikuwa yamefungiwa mifumo hiyo. 

Aidha, akizungumzia eneo la Nishati Safi ya Kupikia, Waziri Ndejembi amesema Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inaendelea na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 - 2034) uliozinduliwa mwezi Mei, 2024, wenye lengo la kuhakikisha angalau asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

“Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kiafya na kimazingira na kuwezesha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa wananchi na katika taasisi hususan, zinazohudumia watu zaidi ya 100,” amefafanua Waziri Ndejembi.

Amesema kuwa kutokana na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali, matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameendelea kuimarika kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 28.6 ya watanzania wenye nishati safi ya kupikia mwaka 2025, hatua ambayo amesema inachangia katika kupunguza uharibifu wa mazingira dhidi ya matumizi ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia na pia kulinda afya za wananchi dhidi ya matumizi ya nishati zisizo safi za kupikia.

“Kwa namna ya kipekee, nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongea Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa maono na uongozi wake uliotuwezesha kuwa na mwelekeo huu wa kitaifa wa kuhakikisha wananchi wetu wanatumia nishati safi ya kupikia, ajenda ambayo imempa heshima ya kuwa kinara wa nishati safi ya kupikia Barani Afrika na kimataifa,” amesema Waziri Ndejembi.

Kwa nyakati tofauti wakichangia katika hotuba hiyo ya Nishati, wabunge waliipongeza REA kwa hatua iliyofikia ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme na miradi ya nishati safi ya kupikia sambamba. 

Mwisho
 

0/Post a Comment/Comments