WAKAZI BUNJU NA MBWENI WAHIMIZWA KUPANDA MITI YA PASAKA

.....

Dar es Salaam

Wakazi wa kata za Bunju na Mbweni wamehimizwa kushiriki kikamilifu katika zoezi la upandaji miti ya Pasaka litakalofanyika katika mitaa yao, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira.

Wito huo unawahusu pia walimu, wanafunzi pamoja na wazazi, ambao wametajwa kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha zoezi hilo na kujenga utamaduni wa utunzaji wa mazingira kuanzia ngazi ya familia hadi jamii kwa ujumla.

Akizungumza katika maandalizi ya zoezi hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Boko Chama, Bw. Beliko Mkute, amesema kuwa wananchi wa eneo hilo wako tayari kushiriki kikamilifu katika upandaji miti popote utakapofanyika.

“Tunawahamasisha wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hili muhimu kwa mustakabali wa mazingira yetu. Tupo tayari kushirikiana na wadau wote kuhakikisha tunapanda na kutunza miti kwa ufanisi,” alisema Bw. Mkute.

Akizungumzia tukio hilo, Balozi wa Mazingira, Bw. Moses Mwakibolwa, amesema kuwa jamii haina budi kubadilisha mitazamo yake ili kuendana na hali halisi ya mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kujitokeza.

Amesema kuwa hali ya hewa imebadilika kwa kiasi kikubwa, hivyo kuna umuhimu wa dhati kwa jamii kupanda miti na kuitunza kikamilifu hadi ikue, ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, ametoa wito kwa wadau na mamlaka husika kuhakikisha upatikanaji wa miti ya matunda, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza hamasa kwa jamii, hususan vijana, kushiriki kikamilifu katika upandaji na utunzaji wa miti.

Zoezi la upandaji miti ya Pasaka linatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na kuchangia katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.









0/Post a Comment/Comments