Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) pamoja na Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), vimezitaka mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto za msongamano bandarini kufuatia kuongezeka kwa shehena ya mizigo katika Bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga.
Akizungumza, Rais wa TAFFA, Edward Urio amesema ongezeko hilo la mizigo ni neema kubwa kwa uchumi wa nchi, lakini limekuja sambamba na changamoto mpya zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.
Amesema mafanikio hayo yalianza kuonekana mwezi Desemba mwaka jana baada ya waendeshaji wa gati namba sifuri hadi saba, kampuni ya DP World, kuweka rekodi ya kushusha takribani makontena 34,000 TEUs ndani ya mwezi mmoja, jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya Bandari ya Dar es Salaam.
Urio amesema kampuni ya Adani nayo imeongeza kasi ya upakuaji wa mizigo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), hali iliyoongeza ufanisi lakini ikaibua changamoto ya uwezo mdogo wa bandari kavu (ICD) kupokea mizigo hiyo.
“Bandari kavu nyingi bado zina uwezo uleule wa zamani licha ya ongezeko kubwa la mizigo. Hali hii inasababisha ucheleweshaji wa kuhamisha makontena kutoka bandarini kwenda ICD, na mwishowe mawakala wa forodha pamoja na wafanyabiashara kuingia gharama za ziada,” amesema Urio.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TATOA, Elias Lukumay, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono ya kuleta wawekezaji kama Adani na DP World, akisema hatua hiyo imeongeza ushindani na idadi ya mizigo bandarini.
Hata hivyo, amesema changamoto zilizopo zisipotatuliwa kwa wakati zinaweza kuwafanya wateja kuikimbia Bandari ya Dar es Salaam kutokana na gharama kubwa za storage na damages.
Lukumay amependekeza kuanzishwa kwa mfumo wa partial release, ambapo sehemu ya makontena yaliyosafirishwa kwenda ICD yanaweza kutolewa moja kwa moja bandarini endapo tayari yamekamilisha taratibu za forodha.
Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano, kuharakisha utoaji wa mizigo na kupunguza gharama kwa wafanyabiashara bila kusubiri makontena yote kufikishwa ICD.









Post a Comment