Na Carlos Claudio, Dodoma.
Wanawake wametakiwa kufanya maandalizi ya kina kabla ya kuingia katika maombi ili kuhakikisha maombi yao yanakuwa na tija, yanasikiwa na kuleta majibu yanayoendana na mahitaji yao ya kiroho na kijamii.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Mwanzilishi na Rais wa GLOWMA, Mtume Pof. Margareth Kilimali, katika siku ya pili ya kongamano la kwanza la wanawake lenye kaulimbiu ya “Wito Maalum kwa Wanawake: Utumishi wa Pamoja kwa Umoja, Mshikamano, Upendo na Amani”, linaloandaliwa na huduma ya Global Women Ministry Africa (GLOWMA).
Akizungumza katika kongamano hilo, Prof. Kilimali alisisitiza kuwa maombi yenye tija hayawezi kufanyika bila maandalizi madhubuti, akieleza kuwa muombaji anapaswa kuelewa kwa kina kile anachokiomba na kuwa na utayari wa kiroho kabla ya kumwelekea Mungu.
Alifafanua kuwa zipo siri mbalimbali zinazowezesha maombi kuwa na matokeo chanya, ambapo mojawapo ni maandalizi. Alibainisha kuwa mtu anayezingatia kanuni hizo hupokea majibu ya maombi yake kwa ufanisi zaidi na maisha yake hubadilika kwa namna isiyo ya kawaida.
“Maombi siyo jambo la kufanya kwa mazoea. Lazima muombaji ajipange, ajitambue na aelewe anachokwenda kukiwasilisha mbele za Mungu. Bila maandalizi, maombi mengi hukosa tija,” alisema.
Aidha, alieleza kuwa dhana ya “tija” haipo tu katika maombi bali pia katika nyanja mbalimbali za maisha, akifananisha na shughuli za ujasiriamali ambapo mtu hupata matokeo kulingana na juhudi na maandalizi anayoweka.
Prof. Kilimali aliongeza kuwa kila aina ya utumishi uwe ni wa kiroho au wa kijamii unahitaji maandalizi ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa. Alitaja mifano ya huduma mbalimbali zikiwemo ujasiriamali, kilimo, afya na elimu, akisisitiza kuwa zote ni huduma kwa jamii na zinahitaji nidhamu pamoja na maandalizi ya kutosha.
“Haijalishi unafanya kazi gani, iwe ni mkulima, mjasiriamali, daktari, mwalimu au mchungaji, yote hayo ni huduma kwa jamii. Na kila huduma inahitaji maandalizi ili iweze kuleta matokeo yenye tija,” alisisitiza.
Katika hitimisho lake, aliwataka washiriki wa kongamano hilo kujifunza na kuzingatia kanuni za maandalizi katika maombi na katika maisha yao ya kila siku ili waweze kufikia mafanikio na malengo waliyojiwekea.








Post a Comment