Na Carlos Claudio, Dodoma.
Wizara ya Katiba na Sheria imeomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuidhinisha jumla ya shilingi bilioni 774.79 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuboresha upatikanaji wa haki nchini.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti bungeni jijini Dodoma Aprili 24, 2026, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema fedha hizo zitatumika kugharamia shughuli za Wizara, Mhimili wa Mahakama pamoja na taasisi zake, kwa lengo la kuhakikisha utoaji wa haki unakuwa wa haraka, wa haki na wenye ufanisi zaidi.
Katika mgawanyo wa bajeti hiyo, shilingi bilioni 636.56 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida, huku shilingi bilioni 137.42 zikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo, hususan katika kuboresha miundombinu na huduma za kisheria nchini.
Dkt. Homera amesisitiza kuwa mojawapo ya vipaumbele vikuu vya wizara hiyo ni kusogeza huduma za msaada wa kisheria hadi ngazi ya jamii. Hatua hiyo inalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi, hasa waishio vijijini na maeneo ya pembezoni ambao mara nyingi hukosa huduma hizo muhimu.
Aidha, wizara imepanga kuandaa Sera ya Taifa ya Haki Madai pamoja na Mpango Kabambe wa Sekta ya Sheria, ikiwa ni jitihada za kuweka mfumo thabiti, wa kisasa na unaoratibu utoaji wa haki kwa ufanisi zaidi nchini.
Katika kuongeza uelewa wa sheria kwa wananchi, serikali imepanga kutoa elimu kwa wadau na umma kuhusu sera za haki jinai na huduma za msaada wa kisheria. Sambamba na hilo, kampeni za elimu ya Katiba na uraia zitaimarishwa ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao na wajibu wao kwa taifa.
Vilevile, wizara inalenga kuimarisha matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro (ADR), hatua itakayosaidia kupunguza msongamano wa kesi mahakamani na kuharakisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.



Post a Comment