Na Carlos Claudio, Dodoma.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma limetoa tahadhari kwa wananchi kuchukua hatua za kujikinga na majanga katika msimu huu wa sikukuu na kipindi cha mvua, likisisitiza umuhimu wa kuwa makini wanaposhiriki shughuli mbalimbali za starehe pamoja na matumizi ya vyombo vya moto.
Tahadhari hiyo imetolewa leo Aprili 3, 2026 jijini Dodoma na Kaimu Kamanda wa Jeshi hilo mkoani hapa, Mrakibu Rehema Menda, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu takwimu za matukio ya majanga yaliyotokea kuanzia Januari hadi Machi 2026.
Menda amesema katika kipindi hicho, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limepokea jumla ya matukio 29 ya majanga mbalimbali, mengi yakihusisha maokozi ya majini kutokana na athari za mvua zinazoendelea kunyesha.
Amefafanua kuwa kati ya matukio hayo, 14 yalitokana na wananchi kujaribu kuvuka mito yenye maji mengi na yanayotiririka kwa kasi, hali iliyosababisha vifo vya watu 17 huku manusura wawili wakiokolewa.
Aidha, amesema matukio matatu yalihusisha watu kuzama kwenye mabwawa, madimbwi na visima, ambapo watu 11 walipoteza maisha bila manusura kuokolewa.
Katika tukio lingine, kaya 49 ziliathirika baada ya upepo mkali unaotokana na mvua kuezua mapaa ya nyumba zao, huku matukio matatu ya kuanguka kwa kuta za nyumba yakiripotiwa na kusababisha vifo vya watu wanane.
Kwa upande wa mafuriko, Menda amesema Jeshi hilo lilipokea matukio sita ya maji kuzingira makazi ya wananchi, ambapo kaya 924 ziliathirika na kati ya hizo, kaya 693 zilisombwa na maji, na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali.
Pia, matukio mawili yalihusisha waendesha vyombo vya moto waliovuka mito bila tahadhari katika Wilaya ya Chamwino, na kusababisha vifo vya watu wawili pamoja na kuharibika kwa magari mawili.
Kwa ujumla, amesema matukio hayo 29 yamesababisha vifo vya watu 49, huku wilaya za Chamwino na Bahi zikitajwa kuathirika zaidi na mvua hizo.
Ameeleza kuwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilifanikiwa kufika katika maeneo yote yaliyopata majanga na kufanya operesheni za uokoaji kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na kuokoa maisha ya wananchi, mali zao na nafaka zilizokuwa hatarini kuharibiwa.
Jeshi hilo, kwa kushirikiana na viongozi wa wilaya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, lilitoa msaada wa haraka kwa waathirika kadri ilivyowezekana.
Kutokana na hali hiyo, Menda amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuepuka kuvuka mito yenye maji mengi, kutopima kina cha maji kwa macho, pamoja na kuwa waangalifu wanapokuwa katika shughuli za kuogelea au starehe.
Vilevile, amesisitiza wananchi kuepuka matumizi ya vilevi kupita kiasi, hasa wanaposhughulika na vyombo vya moto au wanapokuwa kwenye maeneo ya maji, ili kuepuka ajali zisizo za lazima.







Post a Comment