AREPTA YASEMA SHERIA YA MILKI ITAPUNGUZA UTAPELI WA ARDHI

..............

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Serikali imewataka wataalamu wa sekta ya ardhi nchini kuzingatia maadili, uwajibikaji na uweledi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza uaminifu kwa wananchi pamoja na kudhibiti mianya ya rushwa katika utoaji wa huduma.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Kamishna wa Ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Matheus Mhonge wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka na Kongamano la Chama cha Wataalamu wa Sekta ya Milki Tanzania (AREPTA) 2026.

Mhonge amesema Serikali itaendelea kusisitiza uzingatiaji wa maadili ya kazi sambamba na kuhakikisha wataalamu wa sekta hiyo wanatoa huduma kwa kuzingatia sheria, kanuni na maslahi ya wananchi ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika sekta ya ardhi.

Aidha, amesema ipo haja kwa chama hicho kutafuta njia shirikishi za kuhamasisha mitaji kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ya ardhi na majengo ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kusaidia kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ya taifa.

Akizungumza katika kongamano hilo, Rais wa AREPTA, Boniphace Yumba amesema bado kuna changamoto kubwa ya uwepo wa madalali wa ardhi wasiokuwa na usajili ambao wamekuwa wakifanya shughuli za milki bila kufuata taratibu za kitaaluma, hali inayochangia kuharibika kwa taswira ya sekta hiyo pamoja na kuongeza migogoro na malalamiko kutoka kwa wananchi.

Yumba amesema hata baadhi ya madalali waliosajiliwa wanapaswa kufanya kazi chini ya usimamizi wa wataalamu wa sekta ya milki ili kuongeza uwajibikaji na kulinda wananchi dhidi ya utapeli na hasara zinazoweza kujitokeza katika miamala ya ardhi na majengo.

“Sheria ya udhibiti wa milki itasaidia shughuli zote zinazohusiana na milki kusimamiwa kitaalamu na kwa mujibu wa sheria. Bila sheria hiyo, hatari nyingi zitaendelea kuwepo na wananchi wataendelea kupata athari katika sekta hii muhimu ambayo ni uti wa mgongo wa maendeleo ya taifa,” amesema Yumba.

Kwa upande wake, Katibu wa AREPTA, Linda Msaki amesema mkutano huo unatarajiwa kutoka na maadhimio yatakayosaidia kufanikisha ndoto ya muda mrefu ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Milki nchini.

Msaki amesema ajenda hiyo ni miongoni mwa mambo makuu yanayojadiliwa katika kongamano hilo sambamba na mikakati ya utekelezaji wa mfumo wa uchangiaji wa pamoja katika uwekezaji wa milki, hatua inayotajwa kuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa.

Naye Kamishna wa Ardhi, Nathaniel Nonge aliyemwakilisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, amesema Serikali inatambua changamoto zilizowasilishwa na wadau wa sekta hiyo na ipo tayari kushirikiana nao katika kuhakikisha mfumo wa usimamizi wa sekta ya milki unaimarishwa.

Amesema hatua za kuanzisha chombo cha usimamizi wa sekta hiyo zinaendelea vizuri huku Serikali ikiendelea kulifanyia kazi suala hilo kwa karibu ili kuhakikisha sekta ya milki inakuwa na usimamizi wenye tija unaolinda maslahi ya wananchi pamoja na wawekezaji.

Kongamano la AREPTA 2026 linafanyika chini ya kaulimbiu isemayo; “Uchangishaji wa Mitaji kwa Umma katika Uwekezaji wa Sekta ya Ardhi na Majengo: Mkakati wa Kufikia Dira ya Tanzania 2050”.




 

0/Post a Comment/Comments