WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Kakurwa ameongoza kusanyiko la wajumbe wa Taasisi ya Maendeleo ya Mkoa wa Kagera, (KADEFO) huku akitaja jitihada za serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuufungua kimaendeleo Mkoa wa Kagera kupitia uendelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati.
Pia, amempongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya KADEFO, Balozi Liberata Mulamula, viongozi wengine na wanachama wa jumuiko hilo kwa kuimarisha taasisi hiyo na kudumisha umoja kwa wananchi kwa lengo la kuchochea maendeleo ya mkoa huo huku akisisitiza uwajibikaji katika utekekelezaji wa mikakati yao ili kufikia malengo.
Balozi Dk. Kakurwa ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na wajumbe wa KADEFO, iliyowakutanisha Wanakagera kwa lengo la kujadili na kuhamasisha maendeleo ya mkoa huo.
Ametaja mikakati hiyo ya serikali ya kuendeleza mkoa huo ni ujenzi wa tawi la Chuo kikuu cha Dar es Salaam,(UDSM) fursa za ufugaji kupitia uwekezaji wa ranchi, kuimarisha upatikanaji chakula, uvuvi wa kisasa, kilimo na kuimarisha viwanda vya usindikaji, kuunganisha katika gridi ya Taifa ya umeme.
Amesema dhamira ya Rais Dk. Samia ni kuona Kagera ikifunguka kiuchumi kwasababu ya fursa hizo za maendeleo zilizopo na kupakana na mataifa mengine ikiwemo Uganda, ndiyo maana jitihada za makusudi za uwekezaji zinafanyika.
“Mkakati mwingine wa kuendeleza Kagera ni ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa, hali itakayochochea maendeleo zaidi, huku stendi na soko vikiwa vimejengwa na miundombinu ya barabara ikiwa inajengwa, kujenga hospitali kubwa ya kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza,"alisema.
Awali akifungua jumuiko hilo la KADEFO, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya taasisi hiyo, Balozi Liberata Mulamula, alitaja lengo la taasisi hiyo ni kudumisha umoja na kuweka mikakati ya kuendeleza mkoa huo kiuchumi kwa kuvutia wawekezaji kwa fursa zilizopo.
Alitaja baadhi ya manufaa yaliyopatina katika taasisi hiyo ni pamoja na kutoa mafunzo ya matumizi ya teknolojia IT, kwa vijana wa mkoa huo, kuwaunganisha wanakagera, na kufanikisha majumuiko mbalimbali ya KADEFO na kuandaa mradi wenye thamani ya sh.milioni 300 utakao anza kwa michango ya wajumbe.
Alimshukuru mgeni rasmi, Balozi Dk. Bashiru kwa kukubali mwaliko huo, jambo ambalo limewapa heshima kubwa huku akiwashukuru wajumbe wote waliojitokeza na kutoa maoni yao mbalimbali katika kuendeleza mkoa huo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Nazir Karamagi, alisema mkoa huo unazofursa nyingi za uwekezaji ni wakati muafaka wa wanakagera wenyewe kuwekeza kuvutia wengine, hali itakayosaidia kuinua uchumi huku akipongeza uongozi wa KADEFO, kwa jitihada kubwa za kuwakutanisha wanakagera wote, na pendekezo zuri la mradi.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahaya Kido, aliwapongeza wajumbe wa taasisi hiyo walioudhuria jumuiko hilo, huku akipongeza dhamira na jitihada zao za kukwamua mkoa huo na kuweka wazi utayari wake wa kushirikiana na wananchi wa mkoa huo kuchochea maendeleo.
Akiwasilisha salamu za wabunge wengine, Katibu wa Wabunge wa Mkoa huo, Florent Kyombo,ambaye ni mbunge wa Misenyi alisema wote wamefurahishwa na kufanyika kusanyiko hilo na walishiriki katika maandalizi, huku akisisitiza kudumisha umoja na kuchangamkia fursa na kutatua changamoto za mkoa huo.
0000


Post a Comment