Na Zakayo Mosha WAF- Dodoma
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kauli moja limepitisha makadirio ya mapato na Matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Afya yenye jumla ya shilingi Bilioni 1.8 kwa mwaka wa fedha 2026/27 ambayo itasaidia kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya afya.
Wabunge wengi waliochangia hotuba hiyo wamepongeza uamuzi mahususi wa Serikali ya awamu ya Sita kuweka msisisitizo wa Bima ya Afya kwa wote, Ujenzi wa Muhimbili mpya pamoja Uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa viwanda vya ndani vya Dawa kwa lengo la kupunguza utegemezi kutoka nje.
Hayo yamesemwa Bungeni leo Mei 12,2026 katika Bunge la 13, Mkutano wa Tatu, kikao cha 26 cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati Waheshimiwa Wabunge wakichangia mapendekezo ya bajeti ya Wizara ya Afya iliyowasilishwa Bungeni hapo tarehe 11 Mei, 2026 na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa.
"Napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa utashi wake wa kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya mfano katika utoaji wa huduma bora za Afya kwa Wananchi, nawashukuru Wabunge wote kwa jinsi mlivyochangia michango yenu ya mawazo na kutoa ushauri wa kina kwa Serikali kupitia Wizara ya Afya.
"Michango yote tumeichukua na kuifanyia kazi katika utekelezaji wa bajeti hii mliyopitisha kwa lengo la kuhakikisha Nchi yetu inaendelea kuwa Kitovu kikuu cha Tiba utalii kwa Nchi za Afrika Mashariki," amesema Waziri Mchengerwa
Akichangia hotuba hiyo, Mhe. Elibariki Kingu Mbunge wa Singida Magharibi (CCM) ameishauri Serikali kuongeza bajeti ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba ngazi ya msingi kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi wanaoishi vijijini, kuendelea kuweka kipaumbele katika bajeti hii kwa kutekeleza hitaji kubwa la wananchi la bima ya Afya kwa wote.
Naye Mhe. Ahmed Shabiby Mbunge wa Jimbo la Gairo mkoa wa Morogoro (CCM), ameishauri Serikali na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchukua tahadhari kwa kuwa kuna watu wachache wanaopinga Uwekezaji wa ujenzi wa viwanda vya ndani vya Dawa na kuwataja watu hao kama maadui wa Taifa.

Post a Comment