DUCE YAWAJENGEA WALIMU MBINU BORA ZA UFUNDISHAJI

Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu wa DUCE, Profesa Florence Kyaruzi,  akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi wa Kuimarisha Maendeleo ya Kitaaluma na Ulezi kwa Walimu (STPDM) unaotekelezwa Tanzania, Kenya na Sudan Kusini.

    ******

Waalimu nchini wametakiwa kutumia rasilimali zinazopatikana katika mazingira yao kufundishia wanafunzi ili kuwasaidia kujitegemea katika kazi pamoja na kuboresha ustawi wao.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu wa DUCE, Profesa Florence Kyaruzi, wakati akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi wa Kuimarisha Maendeleo ya Kitaaluma na Ulezi kwa Walimu (STPDM) unaotekelezwa Tanzania, Kenya na Sudan Kusini.

Profesa Kyaruzi amesema matumizi ya rasilimali zinazopatikana katika mazingira husaidia kufanya ufundishaji kuwa rahisi, wa vitendo na rafiki kwa wanafunzi huku ukiwajengea uwezo wa kujitegemea.

Amesema mradi huo unalenga kuimarisha uwezo wa walimu kwa kuzalisha na kutumia maarifa kuhusu maendeleo ya kitaaluma, uwezo wao wa kujitegemea katika kazi pamoja na ustawi wao kupitia mfumo wa School In-Service Teacher Training (SITT).

Aidha amesema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Dar es Salaam University College of Education (DUCE), HELVETAS, Kibabii University ya Kenya pamoja na University of Juba ya Sudan Kusini chini ya mpango wa Global Partnership for Education Knowledge and Innovation Exchange (KIX).

Profesa Kyaruzi amesema mradi huo wa miezi 30 ulianza Julai mwaka 2024 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026 huku ukihusisha vyuo 21 vya ualimu na shule 105 za msingi katika nchi hizo tatu.

Ameeleza kuwa kupitia mradi huo walimu wamejengewa uwezo katika masomo ya Hisabati, Sayansi na Stadi za Maisha kwa kutumia mbinu ya SITT sambamba na matumizi ya TEHAMA pamoja na kipengele cha GESI kinachohusisha Usawa wa Kijinsia na Ushirikishwaji wa Kijamii.

Kwa mujibu wa Profesa Kyaruzi, tayari wamefanya utafiti wa awali na kutoa mafunzo kwa wakufunzi, viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa, wakuu wa shule pamoja na walimu kutoka shule za mradi ikiwemo Madenge, Temeke, Kibasila, Chang’ombe na Mgulani.

Amesema kupitia mamlaka za serikali za mitaa pamoja na timu za SITT, wameendelea kufuatilia na kutoa ulezi katika utekelezaji wa shughuli za mradi shuleni ili kuhakikisha matokeo chanya yanafikiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Bajeti kutoka Wizara ya Elimu, Upendo Siaga, amewataka walimu kuendelea kuwapa wenzao ujuzi walioupata kupitia mradi huo ili uweze kuenea katika shule nyingine nchini.

Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Bajeti kutoka Wizara ya Elimu, Upendo Siaga.

Pia ameiomba jamii inayozunguka shule zilizonufaika na mradi huo kushirikiana na kutoa sapoti kwa ajili ya kuhakikisha mradi huo unakuwa endelevu na wenye manufaa kwa jamii.

Naye mmoja wa walimu walionufaika na mafunzo hayo amesema elimu waliyoipata itasaidia kuboresha utoaji wa elimu pamoja na kuwafundisha wanafunzi kwa ubunifu na ustadi zaidi.












Kakolwa Mteza -mwalimu wa Shule ya  madenge.
 

0/Post a Comment/Comments