Na Carlos Claudio, Mbeya.
Jeshi la Magereza nchini limeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika utekelezaji wa programu za urekebu wa wafungwa kupitia shughuli za kilimo cha kisasa, huku Gereza la Kilimo Songwe mkoani Mbeya likitajwa kuwa mfano wa mageuzi ya urekebishaji kwa kutumia elimu ya vitendo.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea gereza hilo kujionea miradi na mafanikio ya urekebu wa wafungwa, Mkuu wa Gereza la Kilimo Songwe, ACP Joaness Baitange, amesema gereza hilo limefanikiwa kuwajengea wafungwa ujuzi wa kujitegemea kupitia matumizi ya teknolojia na zana za kisasa za kilimo.
Amesema mazingira ya gereza hilo yanaonesha wazi namna Jeshi la Magereza lilivyojipanga kuboresha urekebu wa wafungwa kwa kuwapatia mafunzo ya vitendo katika kilimo, uendeshaji wa matrekta, mifugo pamoja na shughuli za bustani na mboga mboga.
“Tunazo zana bora za kilimo ikiwemo matrekta na mashine mbalimbali zinazotumika katika shughuli za kilimo. Wafungwa wanapata nafasi ya kujifunza kuendesha matrekta wakati wa kulima, kupanda na kuvuna mazao,” amesema ACP Baitange.
Ameeleza kuwa kwa sasa wafungwa katika gereza hilo wanahusika na shughuli za kuvuna katika shamba la umwagiliaji lenye ukubwa wa hekta 100, huku wengine wakijihusisha na upakachuaji wa mahindi kwa kutumia mashine za kisasa zilizopo gerezani hapo.
ACP Baitange amesema mafanikio ya programu hiyo yanaonekana hata kwa wafungwa waliomaliza vifungo vyao, akitolea mfano wa mfungwa mmoja aliyemaliza kifungo Machi mwaka 2025 ambaye kwa sasa ni dereva wa magari makubwa aina ya semi-trailer yanayosafirisha bidhaa kutoka Afrika Kusini kwenda Tanzania.
“Mwaka jana mwezi wa sita alirejea hapa kuwaona wenzake na kuwapa moyo wa kuendelea kujifunza na kutumia vizuri muda wao gerezani ili wapate ujuzi utakaowasaidia baada ya kumaliza vifungo vyao,” amesema.
Aidha amesema Jeshi la Magereza linaendelea kutekeleza programu ya kisasa ya urekebishaji wafungwa inayohusisha hatua mbalimbali kuanzia mapokezi ya mfungwa, uchunguzi wa afya, ukusanyaji wa taarifa binafsi pamoja na tathmini ya kitabia kupitia kamati maalum ya wataalamu saba.
Kwa mujibu wa ACP Baitange, tathmini hiyo ndiyo huamua aina ya programu anayopaswa kujiunga nayo mfungwa kulingana na uwezo na mahitaji yake, ambapo baadhi hupelekwa kwenye mafunzo ya uendeshaji matrekta, mifugo, bustani au shughuli za kilimo.
Amesema katika mwaka wa kilimo 2025/2026 gereza hilo lililima hekta 600 na kufanikiwa kuvuna magunia 8,544 ya mahindi sawa na tani 768, chakula ambacho kilisambazwa katika magereza ya mikoa takribani 14 nchini.
Kwa mwaka huu, gereza hilo limepanua uzalishaji wake kwa kulima hekta 900 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Jeshi la Magereza kujitosheleza kwa chakula huku likiwapatia wafungwa stadi za maisha na kupunguza gharama za serikali katika kuhudumia magereza.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Kilimo wa Gereza la Songwe, WRD Emmanuel, amesema kutokana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, Jeshi la Magereza limeanza kuelekeza nguvu katika kilimo cha umwagiliaji na matumizi ya teknolojia za kisasa za uzalishaji.
Amesema mwezi Februari mwaka 2026 jeshi hilo lilituma wataalamu nchini Misri kwa ajili ya kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji usiotegemea mvua.
“Tunatarajia kuanzisha kilimo cha kutumia green house na screen house ili kuweza kuzalisha mwaka mzima. Kwa kutumia teknolojia hizi tunaweza kuzalisha mahindi mara mbili au tatu kwa mwaka na mboga mboga kuzalishwa muda wote wa mwaka,” amesema WRD Emmanuel.




Post a Comment