Na Carlos Claudio, Dodoma
Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa mpango wa bima ya afya kwa wote huku ikieleza kuwa utasaidia kupunguza mateso na gharama kubwa wanazokumbana nazo wagonjwa wa figo wanaohitaji uchujaji wa damu.
Akizungumza leo Mei 6,2026 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Kisayansi kuhusu huduma za upandikizaji viungo, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, amesema wagonjwa wa figo hulazimika kufanya uchujaji wa damu mara tatu kwa wiki, ambapo kila kikao hugharimu kati ya shilingi 150,000 hadi 280,000 na kuchukua takribani saa nne.
Amesema hali hiyo ni changamoto kubwa kwa wagonjwa wengi, hivyo mpango wa bima ya afya kwa wote utakuwa mkombozi kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo muhimu bila mzigo mkubwa wa kifedha.
“Kwa wagonjwa ambao figo zao zinaweza kupandikizwa, tunahamasisha kufanya hivyo ili kuwaondoa kwenye adha ya dialysis ya mara kwa mara,” amesema Dkt. Magembe.
Ameongeza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika huduma za kibingwa bobezi, hususan katika upandikizaji wa viungo mbalimbali.
Mbali na upandikizaji wa figo, tayari huduma za upandikizaji uroto kwa wagonjwa wa saratani na magonjwa ya damu zinaendelea, huku mipango ikiwa inaelekezwa kwenye upandikizaji wa ini na moyo.
Kwa mujibu wa Dkt. Magembe, tangu kuanza kwa huduma hizo mwaka 2017 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na baadaye Hospitali ya Benjamin Mkapa mwaka 2018, zaidi ya watu 147 wamefanikiwa kupandikizwa viungo ndani ya nchi.
Amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya, hususan katika huduma za ubingwa na ubingwa bobezi.
“Huduma hizi si rahisi wala si za gharama nafuu, ndiyo maana serikali imekuja na mpango wa bima ya afya kwa wote ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hizi bila kujali uwezo wake wa kifedha,” amesema.
Aidha, amewataka wananchi kuhakikisha wanajiunga na bima ya afya ili waweze kunufaika na maboresho yanayoendelea kufanyika katika sekta ya afya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, amesema kongamano hilo limewakutanisha wataalamu zaidi ya 150 kutoka Tanzania, nchi za Afrika na Ulaya kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha huduma za upandikizaji viungo.
Amesema lengo ni kupanua zaidi huduma hizo, hasa katika upandikizaji wa ini na moyo, pamoja na kuboresha huduma za figo na uroto.
“Hii pia ni fursa ya kuonesha jinsi Serikali ilivyowekeza katika sekta ya afya na kwamba kwa sasa zaidi ya asilimia 98 ya huduma hizi zinapatikana hapa nchini, hivyo hakuna ulazima wa kwenda nje,” amesema Prof. Makubi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika maeneo ya mafunzo, utafiti, vifaa na dawa ili kuendelea kuboresha huduma hizo.
Katika ushuhuda wa mafanikio, mzazi Shani Mgaraganza amesema mtoto wake aliyefanyiwa upandikizaji wa uroto sasa anaendelea vizuri kiafya tofauti na hapo awali alipokuwa akiugua mara kwa mara na kukosa masomo.
Naye mnufaika wa upandikizaji figo, Bw. Richard Masimba, amesema alipata tatizo la figo mwaka 2022 na kulazimika kufanya dialysis kwa miaka mitatu kabla ya kufanyiwa upandikizaji wa figo Desemba 12, 2025 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.
“Nilipata figo kutoka kwa mwanangu aliyojitolea, na baada ya upandikizaji sasa ninaendelea vizuri. Naishukuru serikali kwa huduma hii ambayo imerejesha matumaini ya maisha yangu,” amesema.







Post a Comment