GLOWMA YAWATAKA WANAWAKE KUMSHUKURU MUNGU NA KUDUMISHA UMOJA

..........

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Mwanzilishi na Rais wa huduma ya Global Women Ministry Africa (GLOWMA), Prof. Margareth Kilimali amesema waumini wanapaswa kuendelea kumshukuru Mungu kwa kuwa fadhili zake ni za milele na hakuna nguvu yoyote inayoweza kushinda na ukuu wake.

Akizungumza jijini Dodoma katika kilele cha kongamano la kwanza la wanawake lililoandaliwa na GLOWMA lenye kaulimbiu ya “Wito Maalum kwa Wanawake: Utumishi wa Pamoja kwa Umoja, Mshikamano, Upendo na Amani,”Mtume Prof. Kilimali alisema Mungu ndiye mkuu juu ya miungu yote hivyo waumini hawapaswi kuogopa jambo lolote.

Alisema kuwa kumshukuru Mungu ni msingi muhimu wa maisha ya kiroho na njia ya kupokea majibu ya maombi pamoja na neema kutoka kwa Mungu.

“Fadhili za Mungu ni za milele, na wema wake kwetu sisi ni wa milele. Hatuna budi kumshukuru Mungu siku zote kwa sababu yeye ndiye Mungu wa miungu na Bwana wa mabwana,” alisema Prof. Kilimali.

Aliongeza kuwa hakuna nguvu yoyote ya dunia inayoweza kumtisha mtu anayemtegemea Mungu kwa kuwa yeye ni mkuu kuliko mamlaka zote.

Aidha, aliwataka waumini kuendelea kulitii neno la Mungu na kuishi katika wokovu wa kweli, akisisitiza kuwa wokovu haupatikani kwa nguvu za mwanadamu bali kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Akinukuu maandiko kutoka kitabu cha Warumi 6:17, alisema waumini waliokoka walitii kwa mioyo yao yote na kuikubali elimu ya Mungu waliyopewa, jambo linalodhihirisha uwepo wa mbegu ya utii iliyowekwa ndani yao na Mungu mwenyewe.

“Sisi sote tuliitii sauti ya Mungu, tukamkubali Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Kutii si jambo dogo, bali ni kazi ya Mungu ndani ya mwanadamu,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mtume Prof. Kilimali aliwaapisha viongozi wapya wa GLOWMA Kanda ya Kati walioteuliwa kushika nafasi mbalimbali ikiwemo Mwenyekiti, Mratibu, Mtunza Hazina pamoja na viongozi wengine wa huduma hiyo.

Alisema uteuzi huo unalenga kuimarisha utendaji wa huduma hiyo katika kuwainua wanawake kiroho, kijamii na kimaadili sambamba na kuendeleza mshikamano na amani katika jamii.






 

0/Post a Comment/Comments