*Watoto wanaolazwa wapungua kutoka 32 hadi 7 kwa robo mwaka
Na Augusta Njoji
IDADI ya watoto wanaokabiliwa na utapiamlo mkali katika Halmashauri ya Mji Handeni imepungua kwa kiasi kikubwa, kutoka watoto 32 waliokuwa wakilazwa hospitalini kwa robo mwaka 2024/25 hadi wastani wa watoto watano hadi saba kwa robo mwaka 2025/26.
Mafanikio hayo yanatajwa kuchangiwa na mikakati madhubuti ya utoaji elimu ya lishe kwa jamii inayotekelezwa na Hospitali ya Halmashauri hiyo, ikilenga kupunguza lishe duni hususan kwa watoto.
Akizungumza Mei 5, 2026 katika kikao cha tathmini ya shughuli za lishe kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2025/26, Afisa Tarafa ya Chanika, Julieth Mushi, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, amepongeza juhudi hizo na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa mkataba wa lishe.
Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe pamoja na Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika kuhamasisha jamii kuanzisha bustani za mboga majumbani na kufuga wanyama ili kukabiliana na tatizo la utapiamlo kwa watoto.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Dkt.Hudi Shehdadi, amesema mikakati inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na kushirikiana na Idara za Elimu ya Msingi na Sekondari pamoja na kamati za lishe za kata kuhamasisha upandaji wa miti ya matunda na uanzishaji wa bustani za mboga, huku kila shule ikitakiwa kutenga angalau hekari mbili kwa ajili ya kilimo cha mahindi.
Aidha, amebainisha kuwa juhudi zimeongezwa katika kuhamasisha wajawazito kuhudhuria huduma za afya mapema ili kupata elimu ya lishe pamoja na virutubisho vya madini chuma, hatua inayolenga kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa na uzito pungufu.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2025/26, Kaimu Afisa Lishe wa Halmashauri hiyo, Getruda Kasabaja, amesema jumla ya wazazi na walezi 9,571 wamefikiwa na elimu ya lishe, huku watoto 17,390 wakifanyiwa tathmini ya hali ya lishe.
Ameeleza kuwa kati ya watoto hao, watoto 221 walikuwa na uzito pungufu sawa na asilimia 1.27, watoto 80 walikuwa na udumavu (asilimia 0.4), na watoto 96 walikuwa na ukondefu (asilimia 0.55). Aidha, watoto saba walipatiwa matibabu ya utapiamlo mkali katika kipindi hicho.
Post a Comment