IZO BATTERIES YATAJWA KUCHOCHEA UHIFADHI WA MAZINGIRA, AJIRA


 *****

Kampuni ya Izo Batteries imetajwa kuwa mfano wa uwekezaji wa kizawa unaochochea utunzaji wa mazingira pamoja na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

Mbali na hilo, kampuni hiyo imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania wengi kupitia shughuli zake za uzalishaji na usambazaji wa betri nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Mei 12, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Izo Mahenge alisema kiwanda hicho kinatumia viwango vya kisasa vya uzalishaji vinavyolenga kulinda mazingira.

Alisema moja ya maboresho yaliyopo ni matumizi ya teknolojia isiyotumia maji kwenye utengenezaji wa betri hizo, hatua inayosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Kwa upande wake, balozi wa bidhaa hizo, Doto Magari alisema serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wazawa kupitia uboreshaji wa miundombinu na sera zinazowezesha viwanda vya ndani kustawi.

Alisema hali hiyo imekuwa chachu ya ongezeko la ajira pamoja na kukuza uchumi wa wananchi kupitia sekta ya viwanda.

Doto alisema uwekezaji wa viwanda vya ndani unawasaidia vijana kupata ajira na kujifunza ujuzi wa kazi za viwandani.

Aidha, aliwataka Watanzania kuendelea kuunga mkono bidhaa zinazozalishwa nchini ili kukuza uchumi wa taifa na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa bidhaa bora barani Afrika.







0/Post a Comment/Comments