KAFULILA: UBIA (PPP) NI NGUZO MUHIMU KATIKA KUIMARISHA SEKTA YA AFYA NA UUGUZI


**********

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Kafulila, amesema kuwa ubora wa rasilimali watu kupitia afya na elimu ndio msingi mkubwa wa Tanzania kufikia lengo la kuwa na uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

Akizungumza kupitia mtandao wake wa kijamii wa X katika maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani, Kafulila alisema wauguzi ni mhimili muhimu wa sekta ya afya na maendeleo ya uchumi, kwani wao ndio waliopo mstari wa mbele kuokoa maisha ya wananchi.

“Uuguzi si kazi tu, bali ni wito wa kitume unaohitaji upendo, subira na utu wa hali ya juu. Wauguzi ni daraja kati ya wagonjwa na kupona,” alisema Kafulila.

Alieleza kuwa bila kuwa na jamii yenye afya bora, haiwezekani kuwa na nguvu kazi yenye tija, hivyo kufanya sekta ya afya kuwa msingi muhimu wa ukuaji wa uchumi mkubwa.

Kafulila alisema pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuboresha miundombinu ya afya, upatikanaji wa dawa, vifaa tiba pamoja na kuongeza wataalamu wa afya, bado Tanzania na Afrika kwa ujumla zinakabiliwa na changamoto ya upungufu wa wauguzi.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), uwiano unaopendekezwa ni wauguzi 45 kwa kila watu 10,000, huku Afrika ikiwa na wastani wa wauguzi 18 kwa watu 10,000. Katika nchi zilizoendelea, uwiano huo umefikia wauguzi 100 kwa watu 10,000. Alisema hali hiyo inaonesha wazi kuwa uwekezaji katika sekta ya afya, hususan uuguzi, unapaswa kuongezwa kwa kasi ili Tanzania iweze kufikia malengo yake ya maendeleo ya mwaka 2050.

Kafulila alisisitiza kuwa Serikali pekee haiwezi kubeba mzigo huo, hivyo mchango wa sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha uwekezaji wa afya na maendeleo ya taifa kwa ujumla. Alibainisha kuwa takwimu zinaonesha sekta binafsi inatarajiwa kuchangia asilimia 70 ya gharama za Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha mwaka 2026/27 hadi 2030/31, sawa na zaidi ya trilioni 334 za shilingi za Kitanzania.

Aidha, alisema zaidi ya asilimia 50 ya matumizi ya sekta ya afya nchini yanachangiwa na sekta binafsi, huku takribani asilimia 40 ya vituo vya afya vikimilikiwa au kuendeshwa na sekta hiyo. Kwa upande mwingine, Kafulila alieleza kuwa ili kuboresha utoaji wa huduma za afya na elimu, ni muhimu kuendelea kuimarisha sera za ubia kati ya Serikali na sekta binafsi sambamba na kuhamasisha uzazi wa mpango, kutokana na uhusiano uliopo kati ya ongezeko kubwa la watu na changamoto za umasikini.

“Ni katika juhudi za kuongeza uwezo wa kugharimia sekta muhimu kama afya na elimu kwa wananchi wenye kipato cha chini, tunaendelea kusisitiza umuhimu wa PPP ili Serikali iweze kuelekeza zaidi rasilimali zake katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara lakini yenye umuhimu mkubwa kwa ustawi wa taifa,” alisema.

Akihitimisha ujumbe wake wa Siku ya Wauguzi Duniani, Kafulila alisema wauguzi ni uhai wa sekta ya afya na kwamba uwekezaji kwao ni uwekezaji wa moja kwa moja katika uchumi wa taifa.

“Heri ya Siku ya Wauguzi Duniani. Changamoto ni nyingi lakini tumaini lipo kadri tunavyoendelea kujenga na kufungua uchumi wetu,” alisisitiza.

0/Post a Comment/Comments