********
Mchambuzi wa masuala ya siasa Bw. Michael Kiria, amekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kupitia kikao chake cha kamati kuu kinachoketi Leo Jumamosi Mei 02, 2026, kushughulikia masuala yake yenyewe ikiwa ni pamoja na kukemea vijana wa Chama hicho dhidi ya uvunjifu wa amani na matukio mengine yenye kukiharibia sifa Chama hicho.
Kiria amebainisha hayo leo Ijumaa Mei Mosi, 2026, muda mfupi kabla ya kufanyika kikao hicho cha Kamati kuu ya Chadema, akisisitiza pia umuhimu wa Viongozi hao wa Chadema kutafakari na kuchukua hatua za kiuwajibikaji dhidi ya wanachama wake wanaotajwa kuwa sababu ya ghasia zilizosababisha vifo na uharibifu wa mali za watanzania na za umma wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
"Leo hatutaki mtuletee mambo ya kutuweka roho juu na kuishi kwa wasiwasi kwasababu tumeshaonja hasara na maumivu ya kupoteza wapendwa wetu, kutusababishia majeraha na kupoteza mali zetu nyingi. Karibuni tumuunge mkono Rais Samia na watanzania wote kwa ujumla kwani bila amani hata ninyi hamtaweza kuendelea na shughuli zenu za kisiasa." Amesema Kiria.
Kiria amesisitiza pia umuhimu wa chama hicho kuwaeleza watanzania kuhusu matumizi ya fedha zake hasa zile wanazochangiwa na wapenda demokrasia wa Tanzania, akisisitiza umuhimu wa kutumia fedha hizo kwa malengo kusudiwa ikiwa ni pamoja na kuwaeleza Watanzania kuhusu namna ambavyo fedha hizo zinatumika.
Ameonya pia kuhusu ukosoaji wa ripoti ya Tume ya uchunguzi wa matukio ya ghasia za Oktoba 29, 2025, akisema tabia hizo zinazofanywa na wanachama wa Chadema zimedhamiria kueneza chuki, uchonganishi na uhasama dhidi ya wananchi na serikali, suala ambalo ni hatari kwa mustakabali wa amani ya Tanzania, akibainisha kuwa ni muhimu kwa kila mmoja ikiwemo vyama vya siasa kujitafakari na kuchukua hatua dhidi ya kile kilichomo kwenye ripoti hiyo hasa kwa namna ambavyo Chadema imetajwa kupitia kaulimbiu yake ya 'No reforms, no election', kama miongoni mwa vichocheo vya ghasia hizo za Oktoba 29, 2025.

Post a Comment