KASI YA ONGEZEKO LA WATU CHANGAMOTO DIRA2050- KAFULILA


*****
Leo ni Siku ya Familia Duniani. Familia ndiyo taasisi ya msingi katika ujenzi wa taifa, uchumi na maendeleo ya nchi yoyote duniani.

Akizungumza kupitia Mtandao wake wa kijamii wa X,Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi (PPP-CENTRE) Mhe. David Kafulila amesema moja ya changamoto kubwa zinazokabili familia nyingi nchini ni suala la uzazi wa mpango na ukubwa wa familia usioendana na uwezo wa kiuchumi wa wazazi. Hali hii husababisha ugumu wa kuwalea watoto katika mazingira bora yatakayowafanya kuwa rasilimali watu yenye ubora, uwezo wa kutimiza ndoto zao na kuchangia maendeleo ya taifa bila kutegemea Serikali kwa kiwango kikubwa.

Kwa sasa, Tanzania ina kiwango cha ongezeko la watu kinachozidi asilimia 3 kwa mwaka, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko wastani wa Bara la Afrika wa asilimia 2, pamoja na wastani wa dunia wa asilimia 1.
Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ipo nafasi ya 81 kwa ukubwa wa uchumi duniani na nafasi ya 165 kwa pato la mtu mmoja mmoja kati ya nchi 193 duniani. Hata hivyo, kwa idadi ya watu, Tanzania ipo nafasi ya 20 duniani, na ikiwa kasi ya ukuaji wa watu itaendelea hivi sasa, mwaka 2050 nchi inaweza kufikia nafasi ya 14 duniani kwa idadi ya watu.

Aidha, makadirio yanaonesha kuwa ifikapo mwaka 2100 Tanzania inaweza kuwa miongoni mwa nchi tisa zenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani. Mifano ya mataifa kama China na India inaonesha umuhimu wa kupanga ukuaji wa watu sambamba na maendeleo ya uchumi. China, pamoja na kuwa moja ya nchi zenye uchumi mkubwa duniani, ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kupitia sera ya kudhibiti ongezeko la watu ya “One Child Policy” iliyoanza mwaka 1979/1980. Kwa sasa China ina ukuaji hasi wa watu.

Kwa upande wa India, licha ya kuwa taifa lenye watu wengi zaidi duniani na uchumi wa tano kwa ukubwa, bado pato la mtu mmoja mmoja linaendelea kuwa la chini ukilinganisha na mataifa yaliyoendelea kama Uingereza.
Tanzania imepanga kufikia uchumi wa dola trilioni moja mwaka 2050.

 Hata hivyo, makadirio yanaonesha kuwa ifikapo mwaka huo idadi ya watu inaweza kufikia milioni 137, hali itakayofanya wastani wa pato la mtu mmoja kuwa karibu dola 7,000 kwa mwaka. Iwapo uchumi utaendelea kukua kwa kasi ya sasa ya asilimia 6 pekee, uchumi wa Tanzania unaweza kufikia takribani dola bilioni 380 mwaka 2050. Katika mazingira hayo, pato la mtu mmoja mmoja linaweza kuwa karibu dola 2,770 kwa mwaka, kiwango kitakachoiweka nchi katika nafasi za chini duniani kwa kipato cha wananchi wake.

Ripoti ya Hali ya Umasikini na Maendeleo ya mwaka 2014 ilionesha kuwa ili Tanzania ifikie malengo ya Dira ya Maendeleo katika sekta ya elimu, ilihitajika kuajiri walimu 900,000 kati ya mwaka 2015 hadi 2025, sawa na walimu 90,000 kila mwaka. Hii inaonesha wazi namna ongezeko kubwa la watu linavyoongeza presha katika utoaji wa huduma muhimu kama elimu, afya na ajira.

Kutokana na hali hiyo, kuna umuhimu mkubwa wa kujenga familia zenye watoto wenye maadili, afya bora, maarifa na uwezo wa kushindana katika dunia ya sasa inayobadilika kwa kasi. Watoto wa leo wenye umri wa miaka 15 kushuka chini ndio watakaokuwa nguvu kazi kuu ya taifa ifikapo mwaka 2050 wakati wa kufunga utekelezaji wa Dira ya Taifa.
Changamoto iliyopo sasa ni namna ya kujenga uchumi mkubwa utakaoweza kugharamia huduma bora za afya, elimu na maendeleo ya rasilimali watu. Haya hayawezi kufikiwa kwa kodi na mikopo pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali na Sekta Binafsi kupitia mfumo wa ubia (PPP).
 

0/Post a Comment/Comments